Sakata la wabunge 19 wa Chadema laibuka tena

Sakata la wabunge 19 wa Chadema laibuka tena

Muktasari:

  • Spika wa Bunge Dk Tulia Akson amesema wabunge 19 wa Chadema walioko Bungeni si haramu kwani wasingekuwepo.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chadema waliopo bungeni wapo kihalali.

Hata hivyo amesema anasubiri michakato halali ndani ya chama chao na ngazi zingine ikithibitika hakuna shida atatekekeza takwa la kikatiba.

Novemba 2020 waliapishwa wabunge 19 wa Chadema ambao walizusha malumbano ya namna waliteuliwa na majina yao kupelekwa Bungeni kwani chama chao hakikutoa ridhaa.

Spika Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu februari 14, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na Wahariri na waandishi wa habari wanaoripoti Bunge.

Akijibu swali kuhusu uhalali wa wabunge wao, Spika amesema hadi sasa wabunge hao wapo kwa mujibu wa sheria kwani kila mbunge ni lazima atokane na chama na hao nao wametokana na chama.

Amesema Bunge halioni shida kuwaondoa wabunge na lilishawahi kufanya hivyo katika mabunge yaliyotangulia.

Hata hivyo amesema mchakato wa namna gani walifika Bungeni siyo hoja ambayo Bunge linatakiwa kujibu bali wenye majibu ni tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Dk Tulia amesema taarifa itakayopelekwa bungeni kuhusiana na wabunge hao sharti iwe imekidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kwa kutendewa haki na yeye hatakuwa na shida kwenye maamuzi.