Samia ashauri kuzibana nchi za Ulaya

Nairobi. Rais Samia Suluhu Hassan jana alitumia dakika saba kushawishi viongozi wa Afrika kukubaliana kuzibana nchi za Ulaya ambazo huzalisha gesijoto duniani, kuchangia ufadhili katika mfuko maalumu ili kuiwezesha Afrika inayoendelea kuathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia alisema bara hilo linaendelea kuathirika zaidi na mabadiliko hayo ikiwamo katika uchumi na maisha ya watu wake huku akishauri uzalishaji wa nguvu kazi yenye tija kwenye fursa ya biashara ya kaboni na kuuza nje bidhaa iliyokamilika badala ya malighafi ya madini ya kimkakati.
“Tunapoelekea kwenye COP28, hatuna budi kuinuka kama sauti ya Afrika kuhusu uanzishwaji wa mfuko maalum kwa ajili ya Afrika. Wanapaswa kusema ni asilimia ngapi ya ahadi zao Afrika na sio vinginevyo,”alisema Rais Samia katika Mkutano Mabadiliko ya Tabianchi Afrika 2023.
Mkutano huo unaojadli mbinu, fursa na namna ya ufadhili wa bara hilo katika miradi, ulianza juzi na utahitimishwa leo Nairobi, Kenya ukijenga ushawishi wa pamoja Afrika kabla ya kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi(COP28) huko Dubai Novemba mwaka huu.
Viongozi hao wa Afrika kupitia hotuba zao, walionekana kuwa na ukali wa kuchoshwa na utamaduni wa wazalishaji wa kaboni duniani unaoendelea kuathiri bara hilo bila kuwa na msimamo wa pamoja kudhibiti.
Rais wa Kenya, William Ruto ambaye ni mwenyekiti wa mkutano huo alisema kiwango cha kaboni barani Afrika bado ni kidogo, lakini athari za kibinadamu ziko juu sana, huku akishauri uamuzi wa haraka kudhibiti hasara na uharibifu huo kwa njia ya mifumo sahihi ya kifedha na matumizi ya teknolojia.

Rais, Samia Suluhu Hassan (wa nne)akiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Viongozi wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa kwenye Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika (Africa Climate Summit 23) unaofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) Nairobi nchini Kenya jana. Picha Ikulu
“Tuwekeze katika ubunifu wa teknolojia kuelekea uwekezaji wa viwanda rafiki wa mazingira. Pia, ni kweli tunachangia kidogo, tunaaathirika zaidi lakini sasa hii ni fursa na tujielekeze huko, lazima tuwe macho na wakati mwingine wanaweza kutupofusha (wazalishaji kaboni) kuona picha kubwa zaidi,” alisema Ruto.
Ripoti mpya ya Bara la Afrika kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi (State of the Climate in Africa 2022) waliyozindula juzi inaonyesha zaidi ya watu milioni 110 katika bara hilo waliathiriwa moja kwa moja na mabadiliko hayo na uharibifu wenye thamani zaidi ya Dola8.5 bilioni (Sh20.4trilioni).
Pia, mabadiliko hayo yaliyosababisha vifo 5,000, asilimia 48 vilihusishwa na ukame na asilimia 43 vilihusishwa na mafuriko kwa mujibu wa Hifadhidata ya matukio ya dharura.
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir alishauri mataifa yanayozalisha kaboni kuongeza ufadhili kwa Afrika yenye uwezo wa kufikia malengo ya mkataba huo unaoelekeza kupunguza gesijoto duniani.
Viongozi hao wanakutana Kenya wakiwa ni wanachama katika Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) waliowasilisha michango yao namna gani watasaidia kupunguza joto duniani hadi nyuzi 1.5C.
“Mabadiliko tayari yanatokea, yasipodhibitiwa miongo ijayo kuna hatari, shinikizo kali linatishia uchumi, maisha na asili ya bara hili,” alisema Balozi Josefa Leonel Correia Sacko ambaye ni Kamishna wa Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Bluu na Mazingira Endelevu katika Tume ya Umoja wa Afrika. Awali, Mkuu wa Shirika la Mafuta la Abu Dhabi, Sultan al-Jaber aliyechaguliwa kuwa rais wa COP28, alisema Umoja wa Falme za Kiarabu( UAE) utawezesha Dola4.5 bilioni za Marekani (Sh10.8trilioni) ili kuongeza uwezo wa Afrika katika mpango wa uwekezaji kwenye nishati safi.
Imeandikwa kwa ushirikiano na Bill & Melinda Gates Foundations