Samia: Tanzania ni moja haigawanyiki wala haiuziki
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika moja ya ziara zake nchini
Muktasari:
- Rais Samia aanza ziara Mwanza akieleza kuwa maendeleo yanayofanyika nchini ni kwa ajili ya Watanzania huku akiahidi kuwa atasimama kikamilifu katika kuijenga Tanzania
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa kila maendeleo yanayofanyika nchini ni kwa ajili ya Watanzania yeye akiwa miongoni mwa Watanzania hao.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo muda mfupi baada ya kuwasili jijini Mwanza ambako atakuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja la Busisi.
Akizungumza katika eneo la uwanja wa ndege wa Mwanza amesema Tanzania ni moja haigawanyiki wala haiuziki na hatowaangusha wananchi katika ahadi yake ya kuijenga Tanzania.
“Mama huyu ni mtanzania atafanya kila analoweza kufanya Tanzania iendelee.Tanzania ni moja haigawanyiki wala haiuziki. Kwahiyo ndugu zangu mama ni mtanzania maendeleo yetu ndiyo muhimu kila linalofanyika ni kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
“Tanzania yetu ni moja ulimwengu mzima, hakuna jamuhuri nyingine ya Tanzania hivyo wa kujenga nchi hii ni sisi kwahiyo kama ni wamachinga, wafanyabiashara au upo popote pale kazi yetu ni kujenga nchi yetu. Katika nyanja zote uchumi, kisisasa hata kijamii lazima tuijenge nchi, ahadi yangu sitawaangusha tutajenga Tanzania. Nadhani mmeanza kuona hatua ambazo tumechukua uchumi umekua hakuna atakayeachwa nyuma,” amesema Rais Samia.
Kauli hii ya kiongozi mkuu wa nchi imekuja kipindi ambacho kuna mjadala mkali kuhusu mkataba wa uwekezaji katika bandari ambapo kampuni ya DP World inatarajia kufanya uwekezaji katika bandari zote za kimkakati.