Sarafu ya Sh100 yatolewa kooni kwa mtoto

Muktasari:

  • Wataalamu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, wamefanikiwa kuitoa sarafu ya Sh100 iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto mdogo kwa siku sita

Dodoma. Wataalamu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, wamefanikiwa kuitoa sarafu ya Sh100 iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto mdogo kwa siku sita.

Akielezea tukio hilo,  Daktari bingwa wa masikio, pua na koo wa BMH, Emmerenceana Mahulu, amesema walimpokea mtoto huyo wa miaka miwili Machi 26, 2024.

"Tumefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto kwa siku sita, kwa kutumia kifaa tiba kinachoitwa ‘esophagoscopy’," amesema Dk Mahulu.

Dk Mahulu amesema kuwa sehemu ya koo ilipokuwa imekwama sarafu  ilisababisha uvimbe. Kuhusu namna ilivyokwama Dk Mahulu,  amesema iliacha uwazi kidogo ambapo ilikuwa ikiruhusu vimiminika kama uji, maji juisi kupita.

"Mtoto anaendelea vizuri baada ya matibabu na anaweza kula vizuri kwa sasa. Tumeshamruhusu na tutamuona tena baada ya wiki moja ili kuona maendeleo yake," amesema.

Kwa mujibu wa mama wa mtoto, Juliana Yuda, mkazi wa Kijiji cha Mkoka wilayani Kongwa, amesema mtoto huyo alienda kucheza na wenzake Machi 26, 2024 alirudi nyumbani muda wa mchana akiwa analia.

"Mtoto alikuwa hawezi kula kwa muda wa siku sita, alikuwa anashindia uji, juisi na maji tu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya siku ya Alhamisi," anasema.