Saruji ya taka kuleta unafuu wa bei nchini

Muktasari:

  • Wakati bei ya saruji ikizidi kupaa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kimebuni saruji mbadala itakayomwezesha mnunuzi kupunguza karibu nusu ya gharama.

Dodoma. Wakati bei ya saruji ikizidi kupaa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kimebuni saruji mbadala itakayomwezesha mnunuzi kupunguza karibu nusu ya gharama.

Teknolojia hiyo inakuja wakati bei ya mfuko mmoja wa saruji wa kilo 50 ukiuzwa Sh17,000 kutoka Sh14,500 ya mwaka jana huku tofali moja likiuzwa Sh1,300 badala ya Sh1,100 ya mwaka jana, jijini hapa.

Akizungumza katika Maonyesho ya Kitaifa ya Ubunifu, Sayansi na Teknolojia (Amkisatu), Mhadhiri wa Udsm, Dk Aldo Kitalika alisema saruji hiyo inaweza kutengeneza matofali, vigae na barabara.

“Saruji hii inatengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea na mawe na udongo unaobaki machimboni kutokana na mazingira husika. Ni teknolojia rafiki kwa mazingira kwani hutumi ataka zisizothaminiwa,” alisema Dk Kitalika.

Mhadhiri huyo alisema teknolojia hiyo ikitumika nchini, inaweza kutoa ajira 500,000 kwa vijana watakaonunua taka.

Alisema miongoni mwa sifa ya vifaa vya ujenzi vinavyotengenezwa kwa teknolojia hiyo ni kuvumilia hali mbaya ya hewa ikiwamo nyumba kutovimba kwa mikoa yenye chumvi nyingi ardhini ukiwamo Dodoma.

“Haihitaji muda mrefu kusubiri tofali likauke, ni saa mbili tu baada ya kulifyatua unaweza kulijengea,” alisema Dk Kitalika.

Mfuko wa kilo 50 ya saruji hiyo alisema unaweza wa kufanya kazi sawa na mifuko 40 ya saruji ya kawaida huku vigae vya Sh25,000 vikipatikana kwa Sh11,000 kwakutumia saruji hiyo.

Mmoja wa watu waliohudhuria banda la chuo hicho, Grace Mwakatobe aliiomba Serikali kuiboresha teknolojia hiyo kisha kuisambaza vijijini.

“Ukizingatia kuwa bei ya vifaa vya ujenzi imepanda kwa kiasi kikubwa, wananchi wakihamasishwa kuitumia na upatikanaji ukawa rahisi utasaidia watu wengi kuwa na nyumba bora na za kisasa,” alisema.