Prime
Sefue aeleza kinachokwamisha ukuaji sekta binafsi Tanzania-2
Muktasari:
- Balozi Sefue amebainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam ambapo amezungumzia masuala mbalimbali ikiwamo uzoefu wake katika kufanya kazi na marais wanne tofauti.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue amependekeza njia zitakazoisaidia Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja, ifikapo mwaka 2050, ikiwamo kurasimisha shughuli za Watanzania.
Balozi Sefue amebainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam ambapo amezungumzia masuala mbalimbali ikiwamo uzoefu wake katika kufanya kazi na marais wanne tofauti.
Ameangazia mkakati wa kurasimisha biashara uliofanyika wakati wa Serikali ya awamu ya tatu chini ya hayati Rais Benjamin Mkapa baada ya kufanya utafiti na kubaini sehemu kubwa ya shughuli za wananchi siyo rasmi.
Katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 (Dira 2050), iliyoanza kutekelezwa Julai Mosi, 2026, Serikali imeweka lengo la kukuza uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini.
Akizungumzia lengo hilo, Balozi Sefue anasema ndoto hiyo inawezekana, lakini haitafikiwa kwa kuendelea na mifumo ya zamani ya kutegemea Serikali kama mchezaji mkuu wa shughuli zote za maendeleo.
Anasema Dira 2050 inaweka wazi kuwa sekta binafsi ndiyo itakayobeba sehemu kubwa ya ukuaji wa uchumi, ikitarajiwa kuchangia takribani asilimia 70 ya ukuaji huo.
Anaeleza jukumu la Serikali linapaswa kuwa ni kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kuimarisha utawala wa sheria, kujenga miundombinu, kulinda usalama na kuhakikisha mifumo ya kiuchumi inafanya kazi kwa ufanisi.
“Biashara, uzalishaji na uwekezaji vinafanywa na sekta binafsi. Serikali inapaswa kuwa mwezeshaji, si mshindani wa wafanyabiashara,” anasema.
Hata hivyo, anabainisha kwamba moja ya vikwazo vinavyokwamisha kasi ya ukuaji wa sekta binafsi nchini ni ukubwa wa uchumi usio rasmi.
Anasema Watanzania wanamiliki mali zenye thamani kama vile ardhi, nyumba na biashara, lakini mali hizo haziwezi kutumika kikamilifu katika mfumo rasmi wa kifedha kwa sababu hazina nyaraka zinazotambulika kisheria kama hati.
Anatumia mfano paspoti ya kusafiria kuelezea umuhimu wa urasimishaji wa mali. “Kijijini kila mtu anakujua na anatambua wewe ni nani. Lakini unapovuka mpaka wa nchi unahitaji pasipoti kuthibitisha utambulisho wako. Vivyo hivyo, mali zako zinahitaji nyaraka rasmi ili zitambulike katika mfumo wa kifedha.”
Anafafanua kuwa bila hati au nyaraka rasmi, mmiliki wa mali hawezi kuitumia kama dhamana kupata mikopo ya kuendeleza biashara au kuwekeza katika shughuli za uzalishaji.
“Tunapaswa kufungua thamani iliyofichika katika mali za wananchi. Hii ndiyo mitaji mikubwa ambayo bado haijatumika kikamilifu katika kuchochea ukuaji wa uchumi,” anasema.
Elimu ya fedha, uwekezaji
Mbali na urasimishaji wa mali, Balozi Sefue anasema Tanzania inapaswa kuwekeza katika elimu ya fedha ili kuwawezesha wananchi kufanya uamuzi sahihi kuhusu matumizi na uwekezaji wa kipato wanachopata.
Anatolea mfano Mkoa wa Geita, ambapo shughuli za uchimbaji madini zimezalisha kundi la vijana wenye utajiri mkubwa walioupata ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo, anasema baadhi yao wanashindwa kudumisha utajiri huo kutokana na ukosefu wa maarifa ya uwekezaji na usimamizi wa fedha.
“Wengi wanapata fedha nyingi kwa haraka lakini hawapati elimu ya namna ya kuzizalisha zaidi. Matokeo yake ni kutumia fedha hizo katika matumizi ya anasa badala ya kuziwekeza kama mtaji wa kuzalisha utajiri wa muda mrefu,” anasema.
Kwa maoni yake, elimu ya fedha inapaswa kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kujenga uchumi shindani na jumuishi.
Akizungumzia uwekezaji wa kimkakati, Balozi Sefue anapinga hoja kwamba Tanzania imekuwa ikichelewa kuamua kuhusu baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo.
Anasema tahadhari na umakini katika majadiliano ya mikataba ya uwekezaji vimeisaidia Tanzania kuepuka makosa yaliyofanywa na baadhi ya mataifa yaliyokimbilia mikataba mikubwa bila kuangalia athari zake za muda mrefu.
“Kuna nchi ambazo zilikimbilia mikataba mikubwa na baadaye zikagundua zimepoteza sehemu ya mamlaka yao au hazikupata mgao unaostahili wa faida zinazotokana na rasilimali zao,” anasema.
Mwanadiplomasia huyo anaeleza Tanzania imekuwa ikitumia muda kujenga uwezo wa wataalamu wake ili kuhakikisha mikataba mikubwa inalinda maslahi ya taifa na wakati huohuo kuvutia wawekezaji.
Anasema miradi mikubwa kama ule wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG) inahitaji uwiano kati ya kulinda masilahi ya wananchi na kutoa mazingira yanayovutia mtaji, teknolojia na utaalamu kutoka nje.
“Hatupaswi kuogopa kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa. Tunachopaswa kuhakikisha ni kwamba mikataba yetu inalinda masilahi ya Taifa na kuwanufaisha wananchi kwa kiwango kinachostahili,” anasema.
Balozi Sefue anasema safari ya kuelekea uchumi wa dola trilioni moja haitategemea ukubwa wa rasilimali za Tanzania pekee, bali uwezo wa kuzisimamia kwa nidhamu, kuweka vipaumbele vinavyoeleweka na kujenga mazingira yatakayoiwezesha sekta binafsi kustawi.
Somo kutoka Singapore
Miaka ya 1960, Tanzania na Singapore zilikuwa sawa kiuchumi, lakini sasa Taifa hilo la Asia limepiga hatua kubwa kiuchumi huku ikiboresha miundombinu na maisha ya watu wake kutokana na rasilimali zake chache.
Juni 8, 2026, Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam aliwasili nchini kwa ziara ya siku tatu ambapo katika ziara hiyo, alishiriki mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo viongozi, wataalamu na wanafunzi walipata fursa ya kujifunza historia ya taifa hilo.
Mhadhara huo, ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi, ulilinganisha safari ya maendeleo ya Singapore na Tanzania huku ukiangazia sababu zilizoifanya Singapore kutoka katika hali ya umaskini wa miaka ya 1960 na kuwa moja ya vituo vikuu vya biashara, fedha na teknolojia duniani.
Balozi Sefue ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Uongozi, anasema moja ya maswali aliyoulizwa Rais Tharman ni namna Taifa hilo lilivyoweza kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa kipindi kifupi.
Majibu yake, kwa mujibu wa Sefue, yalikuwa mafupi lakini yenye ujumbe mkubwa, “kwa sababu hatukuwa na chochote.” Kauli hiyo, anasema inaeleza kwa ufupi msingi wa mafanikio ya Singapore.
Kwa kuwa taifa hilo halikuwa na rasilimali za kutegemea, anasema lililazimika kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika watu wake, elimu, ujuzi, teknolojia, nidhamu ya utendaji na upangaji wa kimkakati.
“Sisi tunaweza kuona hiyo kama kauli ya kawaida, lakini ndani yake kuna somo kubwa sana. Singapore ililazimika kutumia akili, maarifa na ubunifu kama rasilimali zake kuu kwa sababu haikuwa na chochote kingine cha kutegemea,” anasema.
Kwa upande mwingine, anasema Tanzania imebarikiwa kuwa na kila aina ya rasilimali muhimu kwa maendeleo ya uchumi, jambo ambalo wakati mwingine limeifanya nchi kushindwa kuamua maeneo ya kuyawekea nguvu kama vipaumbele.
Anasema baadhi ya washirika wa maendeleo wamekuwa wakieleza kuwa changamoto ya Tanzania si ukosefu wa rasilimali, bali ni tabia ya kutaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja bila kuelekeza nguvu katika sekta chache zenye uwezo wa kuleta mageuzi ya kiuchumi.
“Kwa sababu tuna kila kitu, mara nyingi tunajaribu kufanya kidogo kidogo kila mahali. Mwishowe tunashindwa kufikia kiwango cha uwekezaji na nguvu kinachohitajika ili kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi,” anasema.
Kwa mtazamo wake, Tanzania inahitaji kufanya uamuzi wa kimkakati kuhusu sekta chache zitakazokuwa msingi wa ukuaji wa uchumi kwa miongo ijayo.
Anataja uchumi wa buluu, usafirishaji na huduma za lojistiki, viwanda vya kuongeza thamani ya malighafi, pamoja na sekta nyingine zenye uwezo wa kuzalisha ajira, mapato na uwekezaji kama baadhi ya maeneo yanayoweza kupewa kipaumbele maalumu.
Hata hivyo, kwa mtazamo wake, anasema Tanzania haihitaji kuiga Singapore kwa kila jambo, bali kujifunza misingi iliyoifanya ifanikiwe uwajibikaji, nidhamu ya kitaasisi, uwekezaji katika watu na uwezo wa kuamua kimkakati.
“Tukiacha kutaka kufanya kila kitu kwa wakati mmoja na badala yake tukajenga nguvu katika sekta chache za kimkakati, tunaweza kubadilisha utajiri wetu wa asili kuwa ustawi wa kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” anasema.
Itaendelea kesho...