Sera ya Mambo ya Nje yamulikwa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba akibainisha misingi ya sera mpya ya Mambo ya Nje, kwenye kongamano la pili la kutoa mapendekezo ya kuboresha sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba amebainisha misingi iliyoongezwa kwenye sera mpya ya mambo ya nje, yale yahusuyo ulinzi wa uhuru wa kisiasa, mipaka na kujiamulia mambo yake yenyewe, yaendelezwa.

Dar es Salaam. Wadau kutoka kada tofauti nchini, wametoka maoni yao kuhusu sera mpya ya Mambo ya Nje, huku wakionyesha wasiwasi katika suala la hatima ya ajira za watanzania dhidi ya wageni, ulinzi wa maadili ya Taifa, ujio wa teknolojia mpya ya akili bandia (AI) kwenye soko la ajira, elimu na usalama.

Walionyesha wasiwasi huo wakati wa kuchangia mada kwenye kongamano la pili la kutoa mapendekezo ya kuboresha sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001, lililofanyika jana jijini hapa.

Akichangia mada kwenye kongamano hilo, Profesa Anna Tibaijuka, mwanadiplomasia na waziri wa zamani wa ardhi nchini, ameshauri mkakati wa kutayarisha wanadiplomasia na kulinda marafiki wa Tanzania kihistoria.

“Mfano nchi za Nordic zilimshika mkono mwalimu aliposusiwa na mataifa mengine. Kwa hiyo ni tunahitaji umakini wa kuendeleza marafiki,” amesema na kuongeza;

“Pia siaona mkakati wa kutayarisha wanadiplomasia, mafanikio ya nje lazima unahitaji majembe ya diplomasia, wapewe nafasi kwa kuangalia umahiri. Uchumi wa buluu unahitaji utalaamu wa kuelewa sheria za kimataifa zinazoongoza masuala ya Bahari, hivyo ni lazima tuwe na timu ya watalaamu wa diplomasia.”

Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa la Menonite Tanzania, Nelson Kisare ameshauri kuongezwa msingi wa utu, haki na binadamu.

Katiba ya Tanzania inasema ni siasa ya ujamaa na kujitegemea, je sera hii inaenda kusaidia kujenga ujamaa, tunarejea kwenye azimio la arusha?” amehoji Askofu huyo na kuongeza;

“Katiba imetambua utu, nashauri tuongeze kwenye misingi ya sera, baadhi ya wawekezaji husahau suala la utu na haki za binadamu. Pia tujiulize, hizo mila na desturi za kitaifa ni zipi? Ni vizuri tukaelezwa hizo za kitaifa maana kila mtanzania ana mila zake.”

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amesisitiza sera hiyo kutoyumba kwenye maadili ya Taifa, utayari wa kutumia fursa za kidunia kwa njia ya vijana, namna ya kuendesha vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuonyesha msimamo wa masuala ya kidunia.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, kuna umuhimu nchi ikawa na mfumo mzuri ambao utaruhusu kutekeleza yale yanayotakiwa kuuzwa nje.

“Huwezi kuwa na diplomasia ya kiuchumi wakati mazingira ya ndani hayatekelezeki ndani, itategemea zaidi miundombinu na sera za ndani. Bila misingi mizuri ya ndani, ni changamoto kufanikiwa,” amesema na kuongeza;

“Pili, Kuna mambo ya msingi ya kuenzi. Tanzania ina misingi ya kutetea haki kimataifa. Pamoja na kusisitizwa, suala la maadili, misingi mema ya kutetea haki tuendelee nayo. Mfano masuala yanayotokea Gaza.”

Mwenyekiti huyo wa CUF ameeleza kuwa Dunia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kwamba Tanzania inatakiwa kuwa mstari wa mbele.

“Watalaamu wanatueleza miaka 50 ijayo, usawa wa Bahari utaongezeka kwa mita moja au zaidi, na hivyo kuleta madhara makubwa. Kwa hiyo ni muhimu kuwa mstari wa mbele kwa kuwa ni waathirika wakubwa. Pia kufanya tafiti ili mwanadiplosia anapozungumzia, basi awe anajua anachozungumzia,” amesema na kuongeza;

“Kuhusu Kiswahili, ili tunufaike sio kwamba tuwe watalaamu ila watalaamu pia wa lugha nyingine. Los Angeles nimekuta mwalimu kutoka Ghana anafundisha Kiswahili, bila kujifunza lugha nyingine ni vigumu Kiswahili chako kuleta tija.”

Wadau kutoka kada tofauti wakiwa kwenye kongamano la pili la kutoa mapendekezo ya kuboresha sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Aidha Profesa Lipumba amesema vijana wanaongezeka na kwamba kama wataandaliwa vizuri, nchi inaweza kutumia fursa zinazotokea, huku akibainisha kuwa mwaka 2080, jiji la Dar es Salaam litakuwa nafasi ya tatu kwa wingi wa watu Duniani.

Kwa upande wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Richard Kasesela ameshauri sera hiyo kutoa mwelekeo wa kujenga ‘chapa’ ya Taifa.

“Hoja ya kujenga brand ya Tanzania, imekuwa ikipigwa danadana mara linapekewa wizara ya viwanda, utalii, sasa nashauri litambuliwe katika sera hii. Pia sera tutambue mchango wa Tanzania katika kukomboa mataifa mengine,” amesema na kuongeza;

“Kwa sasa kuna vita ya Brics na G7, sisi msimamo wetu ni wapi? Imefikia hatua Brics wameanzisha benki. GDP ya Brics sasa imefikia dola 63 bilioni, imewazidi G7.”

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha ameshauri matumizi ya Watanzania waishio nje ya nchi.

“Idadi ya watanzania nje ya nchi inaongezeka, lazima tunajiandaaje kuwatumia. Pia ukiangalia Balozi zetu na ukilinganisha na za wenzetu, utaona utofauti mkubwa, zile zinasaidia raia wake. Sasa Balozi zetu zinaweza kuwakusanya Watanzania wote huko ili kuchambua namna gani wanasaidia kulinda sura ya Tanzania,” amesema

Baraka Thomas, mshauri wa sera katika Mtandao wa Asasi za kiraia wa masuala ya Mikataba ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji (Tatic), alisisitiza sera hiyo kuonyesha msimamo wa Taifa katika masuala ya kidunia, ikiwamo kulaani matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Katibu wa Jumuiya ya akina mama wa Kiislamu Mkoa wa Dar es Salaam (Juwakita), Subira Mwakibete alishauri umuhimu wa sera hiyo kutambua utambulisho wa Watanzania kwa njia ya vazi maalumu.

Misingi 13 ya sera

Baadhi ya misingi ya sera hiyo ni uhuru wa kujiamulia yenyewe, kukuza ujirani mwema, kukuza ushirikiano wa kiuchumi na washirika wa maendeleo, kutofungamana na upande wowote, kuendeleza umoja wa Afrika na kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada za maendeleo ya kiuchumi, kulinda amani na usalama.

Hata hivyo, akisoma maeneo mengine sita yanayopendekezwa kuongezwa katika misingi hiyo, Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, wa wizara hiyo, Justin Kisoka alisema:
“Kwanza ni kulinda mila na desturi za nchi, msisitizo wa diplomasia ya kiuchumi, uchumi wa buluu, ubidhaishaji wa lugha ya Kiswahili, ushiriki wa diaspora, jinsia na vijana”.

Faida, changamoto

Katika hatua nyingine, Kisoki alisema miongoni mwa mafanikio ya miaka 23 ya utekelezaji wa sera hiyo ya 2001 ni pamoja na kuwa mwenyeji wa taasisi za kikanda, kituo cha usuluhishi wa kikanda, mikutano na mahakama, ushiriki wa kulinda amani duniani.

“Pamoja na mafanikio hayo, kuna changamoto za kutochangamkia fursa za kimataifa, kutotumia ipasavyo lugha ya Kiswahili, uhalifu unaovuka mipaka na za ulinzi za usalama nchi jirani,” alisema Kisoki.