Serikali kuboresha maeneo ya makumbusho
Arusha. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema kiasi cha Sh2.2 bilioni za Uviko-19 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha Makumbusho ya Malikale zimeendelea kuboresha kwa kiasi kikubwa.
Ameyasema hayo leo Machi 16 jijini Arusha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea miradi ya Uviko-19 katika makumbusho ya Azimio la Arusha na elimu viumbe na kueleza endapo Malikale zitaendelea kuboreshwa zinaweza kuutangaza utalii wa nchi kwa kiwango cha juu.
Aidha Masanja amesema kuwa bado maboresho yanahitajika zaidi ili kuweza kuweka historia vizuri ya uhifadhi kwa njia ya Malikale kupitia majumba ya makumbusho yaliyopo nchini.
Amesema makumbusho zinaendeshwa kwa kusuasua kutokana na ufinyu wa bajeti ambapo kwa sasa hivi wamejipanga kuweka kipaumbele katika maboresho mbalimbali ili kuhakikisha makumbusho hayo yanavutia na kuleta watalii wengi zaidi.
"Serikali imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha maeneo yote yaliyosahaulika yanaboreshwa zaidi ili yakawe na maonekano wa kisasa ili kuweza kuongeza mapato na idadi ya watalii wanaotembelea maeneo hayo." amesema
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi makumbusho ya Taifa, Dk Oswald Masebo amemshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika sekta hiyo na wamepokea maelekezo na mapendekezo na watayafanyia kazi kwa ajili ya kujipanga wenyewe na kuzifanyia mazoezi makubwa.
Aidha ameomba kamati hiyo kuongeza bajeti ya kutosha kwa ajili ya shirika ili kuweza kuboresha zaidi miundombinu mbalimbali na kufanya marekebisho makubwa .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa makumbusho ya maazimio la Arusha, Dk Gwakisa Kamatula amesema kiasi cha Sh 112 milioni kilitengwa kwa ajili ya maboresho na ukarabati wa wa Azimio la Arusha ambapo kwa sasa hivi mradi umekamilika kwa asilimia 100.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya elimu viumbe Arusha, Christina Ngereza amesema kiasi cha Sh272 milioni zilitolewa na serikali kwenye Uviko kwa ajili ya miradi minne ya makumbusho ya elimu viumbe Arusha .
Ngereza amesema miradi hiyo ni onesho la Tembo na wanyama watano wakubwa onesho la wanyama aina ya Reptilia, uboreshaji wa maabara ya bailojia na uboreshaji wa stoo ya bailojia.