Serikali kujenga barabara ya kulipia Kibaha- Moro
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa
Muktasari:
- Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali kwa kwa kushirikiana na sekta binafsi wanatarajia kujenga barabara kuanzilia Kibaha mkoani Pwani hadi Morogoro ambayo watumiaji wa barabara hiyo watalazimika kulipia.
Dear es Salaam. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali kwa kwa kushirikiana na sekta binafsi wanatarajia kujenga barabara kuanzilia Kibaha mkoani Pwani hadi Morogoro ambayo watumiaji wa barabara hiyo watalazimika kulipia.
Profesa Mbarawa ameeleza mpango huo leo Jumatano Novemba 16, 2022 wakati akifungua mkutano wa 15 wa wadau wa usafirishaji na uchukuzi unaolenga ufanisi wa kazi na changamoto za sekta hiyo.
Amebainisha watakaoshindwa kutumia barabara hiyo ya kulipia watatumia barabara ya kawaida na majadiliano baina ya makandarasi yanaendelea huku wananchi watakaopisha mpango huo watalipwa fidia.
Amesema sekta binafsi zitashiriki kwenye ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara na reli ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiitangaza Tanzania kwenye nchi mbalimbali kuwakaribisha wawekezaji waje kuwekeza katika miundombinu mbalimbali.
Waziri huyo amesema barabara hiyo ya kulipia watakaotumia itakuwa gari linakwenda kilometa 120 kwa saa hadi kufika mkoani Morogoro.
"Hii barabara itajengwa na mwekezaji ambaye akakuwa anachukua fedha kwa magari yote yanayopitia katika barabara hiyo lengo lake anachukua fedha hizo ili kurudisha gharama zake alizozitumia," amesema Profesa Mbarawa
Amesema wale watakaoshindwa kutumia barabara hiyo watapita barabara ya kawaida.
"Tanzania haina barabara za kwenda mkoani ya express hata moja tangu tupate uhuru hivyo tunaenda kujenga barabara mpya kutoka Kibaha hadi Morogoro yule atakayetaka kulipia atalipa na yule asiyelipia atapita barabara ya kawaida ambapo ataenda mwendo mdogomdogo," amesema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manunuzi na Mikataba Makao makuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroad), Kingdom Mbangula amesema mkandarasi ameshapatikana ambapo atajenga kwa fedha zake huku malipo yake atayopata wakati wa matumizi ya barabara hiyo.
Mbangula amesema barabara hiyo itajengwa njia nne na msimamizi ameshapatikana ambaye atahakikisha wananchi wanaopitiwa na barabara hiyo wanapatiwa stahiki zao.
Amesema usafiri wa barabara hiyo utakuwa wa mwendo kasi, hawategemei magari mengine kukatiza katika hiyo barabara na itakuwa sehemu chache ya kulipia.
"Tunatarajia kuanzia mwakani Aprili au Mei mwaka 2023 mkandarasi atajenga barabara hii kwa pesa zake mwenyewe halafu magari yanayopitia atachukua hela ili aweze kuchukua fedha alizotumia kujenga mradi huo,"amesema Mbangula.
Wakati huo huo, Mratibu masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Wilbert Muruke amesema wao wanafanya kazi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo usafirishaji, anga na majini ambapo wanatoa huduma za hali ya hewa.
Muruke alitolea mfano kabla ya ndege kuruka lazima wafuatee taarifa za hali ya hewa ili iweze kuruka na upande wa miundombinu ya barabara huwezi kujenga bila ya kuwasiliana na TMA.