Serikali kujenga Hospitali ya Rufaa Ukerewe

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza na wananchi wa Kata ya Bukondo alipokwenda kukagua eneo lililoteuliwa na wananchi wa Wilaya ya Ukerewe kwaajili ya kujengwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wilayani humo. Picha na Saada Amir

What you need to know:

Wakazi wa visiwa vya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wataanza kupata huduma za kibingwa za upasuaji baada ya Serikali kuamua kujenga Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa.

Mwanza. Wakazi wa visiwa vya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wataanza kupata huduma za kibingwa za upasuaji, upasuaji wa mifupa, magonjwa ya wanawake na uzazi pamoja na magonjwa ya watoto baada ya Serikali kutarajia kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wilayani humo.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Bukondo itakapojengwa hospitali hiyo leo Alhamisi Juni Mosi, 2023, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema tayari Sh4 bilioni zimetengwa ili kuanza ujenzi huo  mwaka wa fedha 2022/23.

“Leo tumekuja kuona eneo itakapojengwa hospitali baada ya hapa tutaenda kukamilisha michoro ambayo itatupa thamani halisi ya fedha inayohitajika lakini angalau tuna Sh4 bilioni kibindoni za kuanzia na tunataka hospitali iwe nzuri, ivutie lakini iwe na huduma bora,”

“Tutaanza na daktari bingwa katika fani nne; daktari bingwa wa upasuaji, daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa, daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake na daktari bingwa wa magonjwa ya watoto. Lakini maana yake hapo tutahitaji daktari bingwa wa dawa za usingizi, tutahitaji daktari bingwa wa mionzi,”amesema Ummy

Amesema baada ya hospitali hiyo kukamilika huduma za vipimo vya CT-Scan zitapatikana hivyo wagonjwa hawatolazimika kuvuka maji kuzifuata Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Ujenzi wa hospitali hiyo utakuwa mbadala wa ujenzi wa hospitali kama hiyo iliyojengwa wilayani humo baada ya Serikali kuamua majengo yake yatumiwe na Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kisha ijengwe mpya yenye majengo ya ghorofa.

Ambapo Desemba 21, 2022, Waziri Ummy aliunda kamati maalumu ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Thomas Mihayo kufanya uchunguzi wa ujenzi huo ambao uligharimu Sh2.9 bilioni nakubaini thamani ya fedha haiendani na majengo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile ameishukuru Serikali kwa jitihada za kusogeza huduma za Afya kwa wakazi wa wilayani humo akihaidi kutofumbia macho mapungufu yatakayojitokeza wakati wa ujenzi.

“Sasa Serikali inakwenda kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza kwenye mradi wa kwanza. Niwahakikishie wananchi wa Ukerewe tutakuwa na hospitali nzuri yenye huduma zote muhimu, hatutakuwa na haja ya kupanda tena boti kwenda Mwanza kufuata huduma za Afya,”amezema

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amesema uongozi wa mkoa huo utasimamia vizuri ujenzi huo na kuhakikisha unatekelezwa kwa kiwango na wakati ili wananchi wapate huduma iliyokusudiwa huku Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Charlse Mkombe akisema itakapokamilika wananchi kati ya 15 hadi 20 wanaopewa rufaa kwenda kupata matibabu jijini Mwanza watatibiwa hospitalini hapo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Hassan Bomboko ameshukuru Serikali kwa ujenzi huo huku akimuomba Waziri Ummy kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya wilayani humo.