Serikali kujenga kiwanda cha korosho Kilimanjaro
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa bodi ya korosho Tanzania, Francis Alfred akionyesha moja ya mkorosho ambao mbegu zake zimeliwa na wadudu baada ya kokosekana kwa pembejeo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Serikali imesema inafikiria kuwa na kiwanda cha mfano cha ubanguaji wa korosho katika mkoa wa Kilimanjaro kutokana na zao hilo kuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi.
Moshi.Serikali imesema inafikiria kuwa na kiwanda cha mfano cha ubanguaji wa korosho katika Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na zao hilo kuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya korosho nchini, Francis Alfred wakati alipowasili mkoani humo kwa ajili ya kukagua na kuangalia maendeleo ya zao hilo ambalo linalimwa katika wilaya za Moshi, Same na Mwanga.
"Mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa mipya inayozalisha korosho na zao hili limekuwa na mwitikio mkubwa sana na linafanya vizuri, kwa sasa tunafikiria kuwa na kiwanda cha mfano cha ubanguaji wa korosho katika mkoa huu,"amesema Alfred.
"Lengo la bodi ya korosho na Serikali tunataka katika maeneo yote mapya wazalishaji wa korosho wasifikirie kuuza korosho ghafi bali wafikirie kuuza korosho ambayo imeongezwa thamani,"amesema.
Aidha, amesema kwa sasa bodi inaangalia namna ya kushirikiana na halmashauri za wilaya kutatua changamoto ya upatikanaji wa pembejeo katika maeneo mapya ya zao hilo ili liweze kuwa na manufaa kwa wakulima.