Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuongeza nguvu kupunguza vifo vya mama, watoto

Muktasari:

  • Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2016/2017 hadi kufikia 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000.

Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuimarisha huduma za uzazi salama nchini kwa kuhakikisha wakunga na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanawafikia wananchi wengi zaidi, hatua inayolenga kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2016/2017 hadi kufikia 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000.

Akizungumza leo Septemba 18, 2025, wakati wa kupokea vitendea kazi kwa wahudumu wa afya wa Dar es Salaam na Shinyanga, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer, amesema vifaa hivyo vimetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana na Serikali ya Canada kupitia mradi wa Thamini Uzazi Salama.

“Tunaishukuru Serikali ya Canada kwa kuwa mshirika wetu muhimu katika sekta ya afya. Tumepunguza idadi ya vifo vya watoto kwa asilimia 81, hatua kubwa iliyotokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau,” amesema Laizer akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Beatrice Mwilike, amesema tangu mwaka 2011 chama hicho kimekuwa na ushirikiano wa karibu na Serikali ya Canada katika miradi ya afya ya uzazi.

“Mradi huu ni kielelezo cha kuhakikisha kila mama mjamzito anapata huduma salama kutoka kwa mkunga mtaalamu. Mwaka huu pekee tumefundisha wakunga 180 kutoa huduma za dharura kwa wajawazito na watoto wachanga, 90 Dar es Salaam na 90 Shinyanga,” amesema Mwilike.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

“Hii ni ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha afya za wananchi. Ni ukombozi wa kweli kwa kumkomboa mtu tangu akiwa tumboni,” alisema Mpogolo.

Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, amesema nchi yake inajivunia kushirikiana na Tanzania kuboresha huduma za afya.

“Kuwekeza kwa wakunga na wahudumu wa afya ni kuwekeza katika utu, usawa wa kijinsia na mustakabali bora wa familia za Kitanzania,” amesema.

Mradi wa Thamini Uzazi Salama unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali, Global Affairs Canada, UNFPA na wadau wengine wa sekta ya afya.