Serikali sasa kupambana na wadudu waharibifu angani kwa ndege
Ndege ya kwanza ya kuua visumbufu vya mazao Tanzania.
Muktasari:
- Tanzania imepokea ndege ya kwanza maalumu kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya mimea. Ndege hii itatumika kupambana na wadudu waharibifu wa mazao kama nzige, panya, kwelea kwelea, na viwavi jeshi. Hatua hii inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima nchini kwa kupunguza athari za visumbufu hivyo.
Dodoma. Tanzania imepokea ndege ya kwanza maalumu kwa ajili ya kupambana na visumbufu vya mazao, hatua inayowapa wakulima matumaini mapya katika vita dhidi ya wadudu waharibifu wa mazao.
Ndege hiyo, aina ya Thrush 510 P2, yenye uwezo wa ku-beba lita 900 za viuatilifu na kukaa angani kwa hadi saa nne, imepokelewa leo Mei 30, 2025 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, katika Uwanja wa Ndege wa Jiji la Dodo-ma.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege hiyo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema kuwa ndege hiyo ni mkombozi kwa wakulima waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya uvamizi wa wadudu waharibifu mas-hambani, wakiwemo kwelea kwelea, nzige wekundu na wa jangwani, panya, viwavi jeshi, pamoja na wadudu wengine waharibifu wa mazao.
"Kimaumbile nchi ya Tanzania imeumbwa kuwa mazalia ya nzige tena wale wekundu kwa hiyo walipokuwa wakivamia kwenye mashamba tulikuwa tunapata shida ya kupata ndege kwa sababu tulikuwa tunalazimika ku-kodi kutoka nchini Ethiopia na Kenya na tulikuwa hatuzi-pati kwa wakati," amesema Bashe.
Amesema kuwa mazalia makubwa ya nzige hao yana-patikana katika mikoa ya Dodoma, Katavi na Rukwa, hali ambayo ilisababisha uvamizi wa mashamba na kufanya kazi ya kudhibiti wadudu hao kuwa ngumu.
Waziri Bashe ametoa maagizo kwa viwanja vyote vya ndege nchini kuhakikisha vinatenga maeneo maalum kwa ajili ya kuhifadhi ndege hizo pamoja na vifaa vyake.
Amesisitiza kuwa maeneo hayo yawekwe katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati, huku akibainisha kuwa Serikali itaongeza ndege nyingine ili kuimarisha juhudi za kupambana na wadudu waharibifu wa mazao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose-mary Senyamule, amesema kuwa mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa maeneo yanayoathirika zaidi na vi-sumbufu vya mazao.
Ameeleza kuwa ujio wa ndege hiyo umeleta matumaini mapya kwa wakulima ambao awali walikuwa na hofu ya kulima mazao ya chakula kama mpunga, mtama na uwele kutokana na athari za wadudu hao.
Senyamule amesema kuwa wilaya za Bahi, Kongwa, Chemba na Kondoa ni miongoni mwa maeneo ya-nayoshambuliwa kwa kiwango kikubwa na nzige pamoja na ndege aina ya kwelea kwelea, hali inayowakatisha ta-maa wakulima kuendelea kulima mazao ya chakula kama mpunga, mtama na uwele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema kuwa ndege hiyo imenunu-liwa kwa gharama ya Sh6 bilioni kutoka kwenye fedha za Serikali.
Amesema lengo la ununuzi huo ni kuleta mageuzi ma-kubwa katika sekta ya kilimo, hasa katika udhibiti wa vi-sumbufu vya mimea kama panya, nzige, kwelea kwelea na viwavi jeshi.
Amebainisha kuwa ndege hiyo ina uwezo wa kudhibiti hadi ndege aina ya kwelea kwelea wapatao milioni 200 katika halmashauri 18 nchini, hali ambayo inaweza kuo-koa tani milioni 1.4 za mazao ya chakula kama mpunga, mtama na uwele.