Serikali,Sekta binafsi kuendelea kushirikiana makundi maalum yaweze kuzifikia huduma za afya kirahisi
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte na Mkuu wa GSM Foundation, Faith Gugu, wakimkabidhi baadhi ya ya vitu Katibu wa TAS Mkoa wa Dar es Salaam, Gastino Mcheka(kulia), vilivyorolewa na taasisi hiyo leo Februari 26, 2026 jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili makundi maalum yaweze kuzifikia huduma za afya kirahisi.
Ahadi hiyo imetolewa leo Alhamisi Februari 26,2026 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte, alipokuwa akipokea msaada wa Viti mwendo kwa ajili ya vituo vya afya na vifaa saidizi kwa ajili ya makundi ya watu wenye uhitaji kwa mkoa huo vilivyotolewa na taasisi ya GSM Foundation.
Hafla hiyo ya imefanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa Ilala Boma jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa afya wa mkoa, wataalamu wa sekta ya afya, pamoja na wawakilishi kutoka chama cha ualibino Tanzania (TAS)} na chama cha watu wasiiona Tanzania (TLB)).
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na viti mwendo 30 , fimbo maalum 100 kwa watu wasioona na lenzi zakukuza maandishi 100.
Vifaa vingine ni miwani maalumu ya kupunguza mwanga wa jua 100 , kofia 100 zenye ukingo mpana na mafuta maalum ya ngozi 100 kwa watu wenye ualbino kupitia
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhinte ambaye alikuwa mgeni rasmi, amepongeza mchango wa GSM Foundation kwa hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kurahisha huduma za afya kwa makundi hayo.
“Ushirikiano huu unaonyesha namna sekta binafsi inavyoweza kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuboresha huduma za afya.
"Vifaa hivi vitasaidia kwa kiasi kikubwa makundi maalum na wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka,"amesema.
Aidha Katibu Tawala huyo alihimiza wadau wengine kuiga mfano wa GSM ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi wote.
Awali Mkuu wa GSM Foundation, Faith Gugu, amesema msaada huo umetokana na tathmini iliyofanyika Novemba 2025 wakati wa kambi maalumu ya matibabu iliyoandaliwa nao kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Amana.
Kupitia kambi hiyo, Faith amesema ilibainika kuwepo kwa pengo la vifaa saidizi kwa watu wanaoishi na ulemavu, hususan wasiokuwa na uwezo wa kuona na watu wenye ualbino.
Aidha, hospitali zinazohudumia wananchi wengi zilibainika kuwa na upungufu wa viti mwendo ikiwemo Vituo Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Hospitali ya Mabwepande, Hospitali ya Kivule,Kituo cha Afya Kigamboni Hospitali ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Sinza ambavyo ndivyo vitafaidika na msaada huo .
“Hivyo leo tuko hapa si tu kwa ajili ya kukabidhi vifaa, bali ni mwendelezo wa juhudi tulizoanza kupitia kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika mwezi Novemba 2025 ambapo tulibaini changamoto halisi za upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu na pia upungufu wa viti mwendo katika hospitali zenye msongamano wa wagonjwa,"amesema Faith.
Vifaa hivyo vinalenga kuboresha utoaji wa huduma hospitalini pamoja na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kuishi kwa kujitegemea na heshima.
Hata hivyo ameeleza kuwa kupitia msaada huo, wanachangia juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu katika kuhakikisha usawa na upatikanaji wa nyenzo muhimu kwa wote.
Rai yake Mkurugenzi huyo alizitaka taasisi zilizonufaika kuhakikisha vifaa hivyo vinatumtka kwa malengo yaliyokusudiwa na vinawafikia walengwa sahihi ili kuleta matokeo chanya katika jamii.
Kwa upande wake Katibu wa TAS Mkoa wa Dar es Salaam, Gastino Mcheka, amesema wanashukuru kwa msaada huo kwa sababu utawawezesha kufanikisba malengo yao.
Pia Mcheka amesema kwa walichokifanya GSM ni kutimiza kwa vitendo kauli ya kazi na utu kwa kufanya kila.mtu kujisikia fahari kuishi licha ya changamoto za maumbile anazokuwa nazo.
Naye Honorati Ngowi wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Dar es Salaam, amesema fimbo walizopokea ni msaada zaidi ya fedha.
"Fimbo nyeupe tu yenyewe ilivyo inaongea kwa mtu yoyote atakayekutana na asiyeona na kuwa rahisi kupata msaada anapokuwa barabarani,"amesema Ngowi.
Mwisho.