Serikali: Wengi walioenda COP28 wamegharamiwa na sekta binafsi
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania yafafanua kuhusu idadi kubwa ya ujumbe uliokwenda Dubai kushiriki Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), akisema baadhi yao wanajigharamia wenyewe huku wengine wakigharamiwa na mashirika na taasisi za kimataifa.
Dar es Salaam. Serikali imesema karibu nusu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), umegharamiwa na sekta binafsi.
Ufafanuzi huo, umekuja baada ya juzi na jana kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusu idadi kubwa ujumbe wa Tanzania ulioshiriki COP 28 ukilinganisha na mataifa mengine.
Mkutano COP 28 ambao Tanzania ni mwanachama umeanza Novemba 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023, Dubai.
Idadi hiyo iliibua maswali na majadala katika mitandao ya kijamii huku watu wakihoji wingi wa watu hao, wengine walikwenda mbali wakisema hakukuwa na ulazima wa wingi wa watu hao.
Lakini leo Jumapili Desemba 3,2023 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu ya Rais,(Muungano na Mazingira) imesema Watanzania 763 walijiandikisha kushiriki mkutano huo kati yao 391 walitoka wizara na taasisi za Serikali.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa watu 372 walijiandikisha kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, sekta binafsi, vijana na watoto.
“Hata hivyo idadi ya Watanzania wanaoshiriki kutoka Serikalini ni 66 kati yao 56 wanatoka Tanzania Bara na 10 Zanzibar sawa na asilimia 8.7 ya Watanzania waliojiandikisha.
“Sehemu kubwa ya washiriki wanatoka katika sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vijana na watoto ambayo ni 340 sawa na asilimia 45,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa baadhi ya washiriki kutoka wizara na taasisi za Serikali wamefadhiliwa na mashirika ya kimataifa huku wale wa sekta binafsi, taasisi za kiraia, vijana na watoto wanashiriki kwa gharama zao wenyewe, hatua inayonyesha mwamko kwa Watanzania
Msimao wa Tanzania kwenye mkutano huo
Tanzania ilitaja mambo makubwa manne itakayosimamia kwenye mkutamno huo ambayo ni fedha za ufadhili kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi, mfuko wa pamoja wa majanga na maafa, matumizi ya nishati safi na jumuishi na mjadala wa jinsia unaompa mwanamke kipaumbele imetajwa kama misimamo ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kutoka nchini wameshiri mkutano utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 70,000 kutoka nchi takribani 190.
Taarifa iliyotolewea na Ikulu ilibainisha , “Tanzania inaunga mkono hoja ya kuongeza fedha za ufadhili kwa kuzinga tia athari zinazozidi kuongezeka kwa sasa na kuhakikisha ahadi ya nchi zilizoendelea kutoa dola 100 bilioni (Sh250 trilioni) kila mwaka kwa nchi zinazoende-lea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinatimizwa”.
Jambo jingine ni “Kuhakikisha mkutano unaridhia uanzishwaji wa mfuko wa kupambana na majanga na maafa, Kuhakikisha juhudi za kuelekea matumizi ya nishati safi zinakuwa jumuishi na mjadala wa masuala ya jinsia unazingatia maadili ya kitaifa na kijamii na wanawake wanapewa kipaumbele”.