Serikali ya Tanzania yamaliza mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 40
Muktasari:
Serikali ya Tanzania imemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka 40 kati ya wananchi wa kijiji cha Mlangoni na watawa wa Kanisa Katoliki shirika la kazi ya roho mtakatifu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Siha. Serikali ya Tanzania imemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka 40 kati ya wananchi wa kijiji cha Mlangoni na watawa wa Kanisa Katoliki shirika la kazi ya roho mtakatifu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza leo Jumamosi Desemba 19, 2020 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema wananchi zaidi ya 1000 waliokuwa wakimiliki eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 200 wanapaswa kuwalipa watawa hao Sh2000 kwa kila eneo la mita za mraba. Amesema wanatakiwa kufanya hivyo ndani ya miezi sita kuanzia leo.
" Leo tunazika uhasama tuendelee kuheshimiana na kushirikiana..., hawa masista wamekubali haya maeneo ambayo mpaka leo zipo nyumba 298. Serikali imewapimia hii ardhi ili mbaki hapa lakini nyie mnapaswa kuwalipa fidia hawa masista.”
"Hili eneo lililokuwa na mgogoro lenye ukubwa wa ekari 200 tumeliondoa kwenye hati za hawa masista lakini wataendelea kuwa wamiliki, tulichokifanya ni kwamba wale 298 wenye nyumba zao katika eneo hili tunajua majina yao na tumeshawahakiki na kuanzia kesho mtu anaweza kulipa ,"alisema Lukuvi.
Mbali na wananchi hao kulipa fidia, Lukuvi amesema nyumba nyingine 10 ambazo zimepakana na makazi ya watawa hao zitabomolewa na kulipwa fidia.
Mkuu wa shirika hilo, Dorothea Lazaro amesema shirika hilo limeridhia agizo la serikali la kuwataka kuwapa wananchi eneo hilo ambao wanamiliki kihalali ili kuondoa migogoro uliodumu muda mrefu.
"Tunaishukuru serikali ya Rais Magufuli (John) kwa uamuzi huu, kwa kweli tulikuwa hatulali tukihofia kubomolewa nyumba zetu. Uamuzi huu ni mzuri na sisi tutajitahidi tuweze kulipa hizi fidia kwa wakati maana kwenye hiki kijiji tulikuwa hatuelewani kabisa na hawa masista,” amesema Amosi Mushi mkazi wa kijiji cha Mlangoni