Serikali yaagiza mafunzo walimu wanaokiuka maadili

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu) Gerald Mweri
Muktasari:
Serikali ya Tanzania imeziagiza kamati za Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC) kutoa mafunzo kwa walimu ambao wanaonekana kukiuka maadili ya taaluma hiyo na kufanya makosa ya mara kwa mara ili warudi kwenye mstari na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imeziagiza kamati za Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC) kutoa mafunzo kwa walimu ambao wanaonekana kukiuka maadili ya taaluma hiyo na kufanya makosa ya mara kwa mara ili warudi kwenye mstari na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hayo yamesemwa Jumatatu Desemba 6, 2021 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu) Gerald Mweri wakati akizungumza na Kamati za kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi.
“Mafunzo haya mnayoyapata na ninyi mkayatoe kwa walimu wapya huko katika maeneo yenu, lakini pia wapo walimu ambao walishapewa mafunzo lakini bado wamekuwa wakifanya makosa ya kujirudia rudia,nao nendeni mkawaite na kuwapa mafunzo badala ya kukimbilia kuwapa adhabu,”amesema.
Pia amewataka kuwajengea walimu wapya uwezo na wale ambao hawaendi sawasawa kuwapa mafunzo yatakayowawezesha kufanya kazi zao ipasavyo.
Amesema Serikali haipendi mwalimu afukuzwe kazi kwasababu wapo wengine tayari wana uzoefu wa miaka mingi hivyo wangependa wabaki kuendelea kufundisha.
Amesema kamati hizo zinapaswa kuliangalia suala maadili kwa umakini mkubwa na kutoa adhabu inayomstahili mwalimu kulingana na kosa alilolitenda.
Naye Mwenyekiti wa tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Profesa Willy Komba amesema tume imeamua kuendelea kuwapatia watendaji mafunzo ili wajitambue na si kuwaacha walimu wafanye makossa ndio wawaadhibu.
“Ukishamfukuza mwalimu kutafuta mwalimu mwingine wa kuziba pengo ni kazi, hivyo tutaendelea kutoa mafunzo haya kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha” amesema .
Awali, Katibu TSC Paulina Nkwama amewataka wajumbe wa kamati hizo za wilaya kuwa wasikivu kwa kuwa watajifunza mafunzo ambayo yatasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mwisho