Serikali yaanika mafaniko ziara ya India
Muktasari:
- Baada ya kukamilika kwa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India sekta za Afya, Kilimo, Uwekezaji na maji zimenufaika baada ya hati tofauti kusainiwa.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumaliza ziara yake ya kitaifa nchini India, mafanikio ya ziara hiyo yamewekwa wazi huku sekta ya afya, kilimo, uwekezaji, maji zikinufaika.
Mafanikio hayo yamepatikana kupitia kusainiwa kwa hati mbalimbali za makubaliano kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi za nchi hiyo kupitia mikutano mbalimbali iliyofanyika.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika kukuza ushirikiano ni sekta ya ulinzi hasa utoaji wa mafunzo, nishati na madini ambapo nchi hiyo imeonyesha nia ya kutoa wahandisi wa madini.
Kuimarisha ulinzi wa majini, biashara, kujengeana elimu na teknolojia, elimu na mitandao na kuwashirikisha vijana katika masuala ya teknolojia.
Zuhura amesema hayo yatafanyika kupitia hati 15 zilitiwa saini ambapo hati 10 ni baina ya Taasisi za Serikali na tano ni Sekta Binafsi.
“Hati hizo za makubaliano (Taasisi za Serikali) ni kati ya Wizara ya afya na Taasisi za afya za nchi hiyo, makubaliano mengine ni kuimarisha masuala ya kidigitali, ushirikiano wa masuala ya kiutamaduni, kongani za viwanda, kituo cha uwekezaji cha Tanzania kuweka sahihi na Taasisi ya India inayoshughulikia uwekezaji, kushirikana katika ukaratabi wa vyombo vya majini,” amesema Zuhura.
Pia Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) iliingia makubaliano matatu na ile ya India, na TCCIA ya Zanzibar ikiingia makubaliano na chemba ya chakula na kilimo India.
Zuhura amesema pia katika Jukwaa la kwanza la biashara na uwekezaji Tanzania na India lililofanyika pia liliweza kuleta matunda ya kubadilishana kwa hati nyingine nne za makubaliano na nyingine saba kupitia sekta binafsi huku sekta nufaika zikiwa tena ni afya, kilimo, uwekezaji.
Mchanganuo kisekta
Katika afya, Zuhura amesema tayari India imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika kutoa huduma bobezi ikiwemo kupandikiza figo, uloto lakini sasa kumekuwa na majadiliano ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Tanzania kufanya upandikizaji wa Ini.
“Jambo lingine kubwa ni hospitali maarufu ya Apollo nchini India imekubali ombi la Serikali ya Tanzania la kufungua tawi nchini, sasa wagonjwa badala ya kwenda India wanasogezewa huduma za Afya Tanzania,” amesema Zuhura.
Amesema kipaumbele kingine katikia ziara hiyo kwa upande wa Tanzania ilikuwa ni dawa kwani inazalisha kiwango kidogo ikilinganisha na mahitaji na kufanya asilimia 80 kununuliwa kutoka nje huku 60 kati yake zikitoka India.
“Katika hili sasa Tanzania imesisitiza kuwa ni vyema wafamasia wa India kuzalisha dawa hizo nchini ambapo faida itakuwa kwa watu wa Tanzania na nchi jirani. Pia wamekubaliana kuanzisha kituo cha tiba asilia ambacho bado kipo katika mazungumzo,” amesema Zuhura.
Katika kilimo ambayo imeongezewa bajeti kwa kiasi kikubwa, Zuhura amesema kwa sasa uhitaji uliopo ni teknolojia za kilimo, uzalishaji, soko la uhakika na mitaji katika miundombinu katika uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji.
“Katika ziara hii, Tanzania imefanikiwa kupata uhakika wa soko la mbaazi na Rais Samia Suluhu Hassan ameomba kupatiwa mgao wa soko la tani 200,000 kwani India ni mtumiaji wa mbaazi duniani, Tanzania tunakuwa nchi ya tatu kutoka Afrika kupata fursa hiyo ikiwa ni Msumbuji na Malawi,” amesema Zuhura.
Pia Tanzania imewasilisha mahitaji yake katika benki ya Exim nchini India kwa ajili ya mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Ziwa Victoria utakaogharimu Dola 1 bilioni za Kimarekani (Zaidi ya Sh2.505 trilioni) huku ikielezwa kuwa kutekelezwa kwa mradi huo utafaidisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Dodoma, Kagera na Mara.
“Pia Serikali ina mpango wa kunua trekta 10,000 na kujenga vituo maalumu vya vifaa vya kilimo, katika hili imekubaliana na kampuni ya Mahindra na John Deere kwa ajili ya kununua trekta hizo. Na kuweka kipindi cha miezi 12 kuwekwa kwa viwanda vya kuunganisha trekta na kutengeneza vipuri hapa nchini,” amesema Zuhura.
Katika sekta ya maji bila kubainisha kiwango amesema tayari mkopo umetolewa na endapo ukikamilika zaidi ya Watanzania milioni 6 watafaidika na mradi huo kwa kupata maji safi na salama.