Serikali yabuni mfumo mpya ukikaidi kulipa kodi ya nyumba huingii ndani

Muktasari:
- Serikali imebuni mfumo mpya wa 'Smart lock' ili kudhibiti wadaiwa sugu ambao wamekuwa wakisumbua kulipa kodi ya nyumba ambapo ukikaidi kulipa itakuzuia kuingia ndani.
Arusha. Waziri wa Uchukuzi na Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Arusha wamejipanga kuhakikisha wanatumia mfumo maalumu wa kitasa janja (Smart Lock) kwenye nyumba zao ili kudhibiti uwepo kwa wadaiwa sugu ambao wamekuwa wakisumbua kulipa kodi ya nyumba.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Ijumaa, Machi 3,2023 alipotembelea mradi wa jengo la nyumba za TBA uliopo jijini Arusha.
Amesema kuwa, kumekuwepo na changamoto kubwa ya wadaiwa sugu katika nyumba hizo hali inayopelekea kufikishana hadi mahakamani kwa ajili ya kudai pango la nyumba ila kwa kutumia mfumo huo itakuwa ndio mwarobaini pekee wa suala hilo.
"Sasa hivi hatutaki kusumbuana tena na wapangaji wetu ambao hawataki kulipa kwa wakati. Tukitumia mfumo huo maalumu ikifika mwisho wa mwezi tunampa mteja onyo la kulipa kwa muda wa wiki moja, tukiona hajalipa tunampa tena onyo la pili kwa muda wa siku tatu baada ya hapo asipolipa mfumo wa smartlock unafanya kazi yake kila akitaka kuingia ndani inagoma hadi alipie pango la nyumba na hiyo ndio njia nzuri ya kuwabana wadaiwa sugu na kuepukana kusumbuana nao hadi mahakamani,“ amesema Waziri Mbarawa.

Waziri wa ujenzi, Profesa Makame.
Hata hivyo Waziri Mbarawa amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo pamoja na thamani halisi ya fedha zilizotumika kuendana na mradi huo.
Hata hivyo, amesema kuwa mradi huo umefanyika kwa umakini mkubwa na fedha zilizopangwa kutumika katika mradi huo zinaendana na mradi wa jengo hilo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja TBA mkoa wa Arusha, Mhandisi Juma Dandi amesema kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuchukua familia 22 ambavyo ni kitega uchumi cha TBA ambapo wapangaji katika nyumba hiyo watapaswa kulipa kwa wakati kwani wanapokea hela kila mwezi.
Amesema kuwa, mradi wa jengo hilo lenye ghorofa 10 umeshatumia kiasi cha Sh5.2 bilioni hadi sasa ambapo mpaka kukamilika litagharimu Kiasi cha Sh5 .5 bilioni na unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya wiki mbili hadi tatu.
Aidha Mhandisi Juma amesema kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaweza kukidhi mahitaji ya makazi kwa watumishi wa umma na mapato ya serikali kwa ujumla na uwepo wa mradi huo umeweza kuongeza idadi kubwa ya ajira kwa mafundi na wafanyakazi wengine pamoja kuwepo kwa ununuzi mkubwa wa vifaa vya ujenzi.