Serikali yaeleza haja ya kufungamanisha mfumo wa Mahakama na Kimila

- Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu Mkoa Kilimanjaro Tamari Mndeme, akizungumza leo katika maadhimisho ya Siku ya sheria nchini.
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa mfumo wa kimila hurahisisha mchakato wa kutoa haki na hivyo utawezesha kuharakisha mashauri mahakamani.
Moshi. Mwakilishi wa Mwanasheria mkuu wa serikali mkoani Kilimanjaro Tamari Mndeme amesema kuna haja ya kufungamanisha mfumo wa kisheria unotumiwa na Mahakama na mfumo wa kimila au kiasili katika utoaji wa haki ili kupunguza mlundikano wa mahabusu gerezani.
Mndeme ameyasema hayo leo Februari Mosi wakati Mahakama Kuu ikiadhimisha kutimiza miaka 100, ya utendaji wake nchini ikiwa pia ni siku ya maadhimishi siku ya sheria nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Mndeme amesema zipo faida nyingi katika kutatua migogoro kwa kutumia taratibu au falsafa za kimila na kiasili ikiwepo kuunganisha jamii husika.
Amefafanua kuwa gharama katika utatuaji wa migogoro kwa njia ya asili ni ndogo ikilinganishwa na mfumo wa sasa wa mahakama ambapo hutumia gharama kubwa kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwepo kuleta mashahidi, kufungua mashauri, na kuweka mawakili
"Mfumo huu wa asili hutumia muda mfupi ikilinganishwa na mfumo wa sasa ambapo baadhi ya mashauri yanakaa muda mrefu na mwisho kuleta msongamano wa mahabusu magerezani hasa kwa makosa yale yasiyokuwa na dhamana".
Amefafanua kuwa serikali ilifanya juhudi kubwa kuingiza mfumo wa kimila ya utoaji haki, katika sheria ya matumizi ya sheria sura ya 358 ya sheria ya Tanzania ambayo inaruhusu matumizi ya ya sheria za kimila pale ambapo wahusika wa migogoro wanatoka katika jamii iliyojiwekea mfumo wa utatuzi wa migogoro.