Serikali yajitathmini upya utoaji wa mikopo elimu ya juu

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya HESLB, Profesa Hamisi Dihenga amesema kutokana na ongezeko la wanafunzi, haiwezekani kuendelea kuitegemea Serikali kuwekeza fedha za mikopo.

Muktasari:

  • Tangu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ilipoanzishwa mwaka 2005, imeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh5.9 trilioni na iliyorejeshwa ni zaidi ya Sh1.5 trilioni, huku mahitaji ya mikopo yakiendelea kuongezeka.

Dodoma. Wakati Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), ikiwa imeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh5.9 trilioni kwa wanafunzi wa elimu ya juu tangu ilipoanzishwa mwaka 2005, tathmini ya upatikanaji wa fedha inafanyika kutokana na ongezeko la wanafunzi vyuoni.
 
Akizungumza leo Alhamisi Machi 16, 2023  jijini Dodoma katika mkutano wa tathmini ya ulipiaji wa elimu ya juu, Mtendaji Mkuu wa HESLB, Abdul-Razak Badru alisema tangu mwaka 2005 ilipoanzishwa bodi hiyo wanafunzi wanaonufaika na mikopo wameongezeka kutoka zaidi ya 20,000 hadi 70,000.

“Tunachokifanya ni tathmini ya utafutaji wa vyanzo vingine vya mapato, kwa sababu kwa miaka 18 iliyopita wanafunzi walikuwa 20,000, leo tunazungumzia wanafunzi wapya zaidi  ya 70,000 na tunazungumzia uwekezaji wa Sh5.9 trilioni ambazo Serikali imewekeza na mwaka huu peke yake imewekeza Sh654 milioni,” alisema.

Mbali na utafutaji wa vyanzo vipya, alisema pia wanatathmini kozi zinazochukuliwa na wanafunzi kama zinalingana na mahitaji ya soko la ajira.

“Ni kiasi gani hizo kozi zinawiana na mahitaji ya soko la ajira? Hii itaisaidia serikali kuona kama uwezekezaji wake unaiwina na masoko?

“Tunaangalia pia maandalizi ya sekta ya elimu ya juu ya kulipia wanafunzi wanaotokana na mikakati ya Serikali, kama unavyojua kuna elimu bila ada, hivyo kutakuwa na ongezeko la wanafunzi vyuoni. Hivyo tutaangalia maandalizi ya Serikali kutanua ulipaji katika ngazi za astashahada na stashahada,” alisema.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu marejesho ya mikopo hiyo, Badru alisema kwa wastani mikopo hiyo inarejeshwa Sh180 bilioni kwa mwaka likiwa ni ongezeko kutoka Sh30 bilioni zilizokuwa zikilipwa miaka sita iliyopita.

“Kwa ujumla, mikopo iliyotolewa (Sh5.9 trilioni), Sh1.5 trilioni imesharejeshwa, lakini ujue mikopo hii ina iva na hata ikirejeshwa leo yote bado mahitaji yanazidi kuwa makubwa zaidi,” amesema.  

Awali, akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Franklin Rwezimula amesema tathmini hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa ya elimu na yanayfanywa kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

“Kwa sasa chanzo kikubwa cha kusaidia wanafunzi wasome ni Bodi ya Mikopo, lakini kwa mageuzi ttunayoyafanya wanafunzi watakuwa wengi hivyo bodi haitaweza kuchukua wanafunzi wote,” amesema.

Amesema miongoni mwa vyanzo walivyofanikiwa kuongeza ni program ya Elimu Loan ya Benki ya NMB ambayo imetenga Sh200,000 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi hasa wafanyakazi wa Serikali na sekta binafsi kwa riba ya asilimia 9.

“Tuna tathimini pia je elimu inayotolewa inawezeshha wanafunzi kujiajiri? Tuapotoa fedha hizi, lazima tuhakikishe wanafunzi wanapata elimu itakayowezesha kujiajiri,” amesema.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya HESLB, Profesa Hamisi Dihenga amesema kutokana na ongezeko la wanafunzi, haiwezekani kuendelea kuitegemea Serikali kuwekeza fedha za mikopo.