Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yakumbushwa ubia na sekta binafsi kuimarisha elimu ya amali

Mkurugenzi wa Mwanza Polytechnic Institute ya mjini Maswa, Jerry Nyabululu, akizungumza katika mahafali ya stashahada ya uongozi katika elimu yaliyofanyika katika kampasi ya taasisi hiyo mjini Maswa. Picha na Samwel Mwanga.

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanza Polytechnic Institute, Jerry Nyabululu amesema ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu ili kufanikisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya amali kwa kutumia miundombinu iliyopo katika taasisi binafsi.

Maswa. Serikali imekumbushwa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika utoaji wa elimu ili kufanikisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya amali na kutumia kikamilifu miundombinu iliyowekezwa katika taasisi binafsi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 27, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanza Polytechnic Institute, Jerry Nyabululu wakati wa mahafali ya kuwatunuku wahitimu 220 stashahada ya uongozi katika elimu, yaliyofanyika katika kampasi ya taasisi hiyo mjini Maswa.

Nyabululu amesema taasisi binafsi za elimu zipo tayari kusaidiana na serikali katika utekekezaji wa mtaala mpya wa amali.

Amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu, lakini mafanikio ya mtaala mpya yataongezeka zaidi ikiwa kutakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.

Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Esther Marwa (kulia), akimkabidhi cheti mhitimu Baraka Mkama aliyesoma stashahada ya uongozi katika elimu kutoka Mwanza Polytechnic Institute ya mjini Maswa. Picha na Samwel Mwanga.

Amesema mtaala huo unatoa nafasi kwa wanafunzi kuendelea na kidato cha tano na sita au kujiunga na mafunzo ya ufundi, hivyo kuna haja ya kutumia miundombinu iliyopo katika taasisi binafsi ili kuongeza nafasi za kujifunza kwa vitendo.

“Taasisi yetu ina uwezo wa kupokea wanafunzi 1,500 lakini kwa sasa tuna wanafunzi takribani 200 pekee. Tuna maabara, karakana za umeme na vifaa vya kisasa vinavyoweza kutumika kufundishia elimu ya amali,” amesema.

Ameongeza kuwa mbali na kutoa stashahada ya uongozi katika elimu, taasisi hiyo, pia, inatoa mafunzo katika fani za Umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Biashara, Usaidizi wa Maabara, Usimamizi wa Taka za Hospitali, Utunzaji wa Kumbukumbu za Wagonjwa na Uhudumu wa Wagonjwa, hivyo ina uwezo wa kuchangia utekelezaji wa mtaala mpya kwa kutumia wataalamu na miundombinu iliyopo.

“Tunaiomba Serikali iingie nasi katika ubia (PPP) ili wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watumie miundombinu yetu ya elimu ya amali. Tuko tayari kushirikiana na serikali ya mkoa pamoja na Wizara ya Elimu kuhakikisha mtaala mpya unatekelezwa kwa ufanisi,” amesema.

Amesema pamoja na Serikali kuwa na jukumu la msingi la kutoa elimu, haiwezi kutekeleza majukumu yote peke yake, hivyo mchango wa sekta binafsi ni muhimu katika kuboresha ubora wa elimu nchini.

Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Esther Marwa, amesema elimu ni mchakato unaoendelea maisha yote na kwamba mafunzo yaliyotolewa na taasisi hiyo ni sehemu ya elimu nje ya mfumo rasmi inayowapa watumishi nafasi ya kujiendeleza wakiwa kazini.

Amewataka wahitimu kuhakikisha elimu waliyoipata inaleta mabadiliko katika utendaji wao wa kazi, uongozi wa taasisi wanazozitumikia na katika jamii inayowazunguka.

“Kujifunza lazima kuonekane katika utendaji wa kazi na maisha yako. Ninyi ni walimu wa shule za msingi za serikali, hivyo jamii inatarajia kuona matokeo ya elimu mliyoipata,” amesema.

Amewahimiza wahitimu kuwa mabalozi wa kuhamasisha walimu wengine kutumia fursa zinazotolewa na taasisi binafsi kwa ajili ya kujiendeleza kitaaluma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Joseph Omahe amesema halmashauri hiyo haijaitumia kikamilifu taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo walimu wake, lakini itaanza kuhamasisha walimu kujiunga na mafunzo hayo.

Amesema kwa sasa walimu wakuu wa shule za msingi wanatakiwa kuwa na stashahada ya elimu, hususan katika uongozi, ili kuendana na mahitaji ya mfumo wa elimu unaoendelea kuboreshwa.

“Ninaamini wahitimu hawa wameandaliwa kuwa viongozi bora watakaosimamia kwa ufanisi masuala ya kitaaluma katika shule zetu,” amesema.

Baadhi ya wahitimu walisema mafunzo hayo yamewapa maarifa na mbinu mpya za kuboresha utendaji wao.

Baraka Mkama, mwalimu wa shule ya msingi Nyerere jijini Mwanza, amesema elimu aliyoipata itamsaidia kuongeza ufanisi wa kazi na kuboresha matokeo ya wanafunzi anaowafundisha.

Mwalimu wa elimu maalumu katika Shule ya Msingi Kirumba jijini Mwanza, Ruza Tumbo amesema mafunzo hayo yatamuwezesha kuwahudumia vizuri zaidi wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika kazi yake.

Naye, mwanafunzi Mustafa Sadik amesema amepata mbinu mpya za uongozi na ufundishaji ambazo zitamsaidia kuwa kiongozi bora na kusimamia kwa ufanisi shughuli za kitaaluma shuleni.