Serikali yaokoa watoto 335,971 mazingira hatarishi

Muktasari:
- Watoto hao waliookolewa kupitia Serikali za mitaa katika halmashauri zote ni wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, wakiwemo waliotelekezwa, wahanga wa matukio ya ukatili, na usafirishaji haramu wa binadamu.
Arusha. Serikali imefanikiwa kuwaokoa jumla ya watoto 335,971 kutoka katika mazingira hatarishi, wakiwemo waliokuwa wakitoroshwa nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka wizara yenye dhamana ya watoto, Dk Nandera Mhando katika uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka mitano wa shirila la Compassion International Tanzania unalenga kuwanufaisha watoto na vijana milioni 1.7.
Dk Nandera alisema kuwa watoto hao waliookolewa kupitia Serikali za mitaa katika halmashauri zote ni wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, wakiwemo waliotelekezwa, wahanga wa matukio ya ukatili, na usafirishaji haramu wa binadamu.
"Tumeweza kuwasajili watoto 335,971, katika kipindi cha kuanzia julai 2022 hadi April 2023 kati yao wasichana wakiwa 167,337 na wanaume ni 168,634 ambao sasa wanapatiwa huduma muhim kulingana na mahitaji yao," alisema Dk Nandera
Alisema watoto hao wanapatiwa huduma muhimu ikiwemo malazi, mavazi, elimu, matibabu chakula na lishe kupitia katika vituo 344 vya Serikali na wengine wanaoishi katika kaya zao.
"Serikali inatambua mchango wa mashirika haya, ikiwemo Compassion katika kutusaidia kuhudumia watoto walio katika mazingira hatarishi nchini ambao mmeshahudumia 115,000 na sasa mnazindua mpango mwingine wa kwenda kunyanyua wengine milioni 1.7, hakika si kazi rahisi hivyo Serikali tunaahidi kutoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha mnatekeleza kikamifu,"
Awali mkurugenzi wa shirika la Compassion International Tanzania, Merry Lema alisema mpango huo ni mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023-2027 unaolenga kusaidia watoto na vijana milioni 1.7 walio katika jamii hitaji.
"Katika mpango huo tunalenga kuangalia uhakika wa chakula, lishe, elim bora, afya, matibabu, ufundi lakini pia kuongeza kipato cha kaya kujihudumia hasa katika shughuli za ufugaji, kilimo na ujasiriamali,"
Alisema mkakati huo wameuandaa kwa kuzingatia takwimu mbalimbali za kitaifa zikiwemo za changamoto, mahitaji na vipaumbele vya watoto na vijana vilivyoainishwa katika taarifa za serikali, wadau wa maendeleo, taasisi na mashirika tofauti tofauti.
Awali kwa niaba ya viongozi wa dini, Askofu Arnold Manase alisema kuwa jukumu la kusaidia watoto na vijana hao ni la wote hivyo wasiachie shirika wala kanisa pekee.
"Inafaa tuwe na moyo wa kusaidia wahitaji sisi wenyewe sio kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi wakati sisi kuna baadhi ya matukio tunayafanya kwa kufuja pesa ikiwemo harusi za gharama kubwa na hata ubarikio au sikuu za kuzaliwa,"