Serikali yaombwa kuhamasisha bidhaa za ndani

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaji Jabiri Shekimweri (kushoto) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Dar Ceramica Centre, Raymond Nkya wakati wa ufunguzi rasmi wa tawi la Dodoma.

Muktasari:

  • Katika kuhamasisha biashara na uwekezaji nchini, Serikali imeombwa kuhamasisha na matumizi ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani.

Dodoma. Serikali imeombwa kutoa ushirikiano kwa kutumia bidhaa zinazouzwa na wafanyabiashara wa ndani katika miradi inayoendelea jijini Dodoma.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Dar Ceramica Centre, Raymond Nkya katika uzinduzi wa tawi lake jijini hapa.

Amesema wanaimani makandarasi, Serikali na wananchi wanaohitaji vifaa vya ujenzi hawatasafiri umbali mrefu kupata bidhaa hizo za vifaa vya ujenzi vinavyopatikana katika kampuni hiyo.

“Kama tunavyofahamu, Dodoma ndio mji mkuu wa nchi yetu, ofisi zote za Serikali sasa zinapatikana hapa.

“Kumekuwa na miradi mingi sana ya ujenzi na makandarasi wengi na watu binafsi wamekuwa wakiingia gharama kubwa kusafirisha mizigo kutoka matawi yetu mengine nchini kuja Dodoma na mikoa jirani lakini tumekuja na suluhisho,” amesema Nkya.

Amesema uamuzi wa kufungua tawi hilo umesababishwa na maombi mengi kutoka kwa makandarasi na watu wenye miradi ya ujenzi wa nyumba na ofisi mbalimbali.
Nkya amesema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika usambazaji wa tiles, vifaa vya ujenzi vya bafuni na chooni.

Amesema wanaagiza vifaa hivyo kutoka kwa wazalishaji na wasambazaji wa Uropa na China na kwamba kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa wateja katika ukanda wa Afrika mashariki na kati tangu mwaka 1998.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema ujio wa Dar Ceramica Dodoma utachangia miradi inayoendelea kufanyika kwa ubora wa hali ya juu na pia itaongeza mapato kwa njia ya kodi.  

“Tunajivunia kama wana Dodoma kupata tawi la Dar Ceramica, pamoja na upatikanaji wa bidhaa kurahisishwa, ufunguzi huu ni ishara kuwa kutakuwa na ajira za moja kwa moja na ambazo sio za moja kwa moja kwa wakazi wa Dodoma,” amesema Rosemary.

Pia, amesema wakazi wa Dodoma na mikoa jirani sasa hawatapata tena adha ya kusafiri mbali kutafuta bidhaa ambazo sasa zitapatikana Dodoma.