Serikali yaongeza tahadhari ya ugonjwa wa ebola, vifaa kinga na watumishi wa afya

Muktasari:

  • Tahadhari hiyo imechukuliwa baada ya wafanyakazi tisa wa kada ya afya wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kuugua ebola na mmoja kufariki dunia.

Dar es Salaam. Serikali imewaongezea vifaa kinga watumishi wa afya kote nchini hasa maeneo ya mipakani ili kuwakinga na mlipuko wa ebola iwapo utatokea.

Tahadhari hiyo imechukuliwa baada ya wafanyakazi tisa wa kada ya afya wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kuugua ebola na mmoja kufariki dunia.

Akizungumza jana na wanahabari, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali imechukua tahadhari hiyo baada ya watu 91 kuugua ugonjwa huo DRC, huku 50 kati yao wakifariki dunia.

Katika mlipuko wa ugonjwa huo uliotokea Julai, watu 26 waliugua.

“Wafanyakazi hawa wa afya inaaminika kwamba wamepata ugonjwa huu wakati wakiwahudumia wagonjwa katika kliniki zao za kawaida na siyo zile za kutibia wagonjwa wa ebola na wengi wao wameambukizwa kabla ya WHO (Shirika la Afya Duniani) kutangaza mlipuko huu,” alisema.

Alisema takwimu zilizotolewa na WHO zinaeleza kuwa wafanyakazi tisa wa afya wamethibitika kuugua ugonjwa huo. Alisema watumishi wa afya wanapewa maelekezo namna ya kuchukua tahadhari wanapowahudumia wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo.

Waziri alisema Serikali inaendelea kuwaongezea uwezo na mafunzo ya utambuzi watalaamu 80 katika semina inayofanyika mkoani Morogoro.

Alisema mafunzo kwa timu za dharura na maafa yataanza Agosti 27 jijini Mwanza.

“Lengo ni kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuratibu na kukabiliana na ugonjwa huu endapo utatokea hapa nchini. Idadi ya wataalamu watakaopata mafunzo hayo kutoka Mkoa wa Mwanza ni 15, Kagera (15) na Kigoma (15) ili kujaza nafasi ya upungufu katika wilaya ambazo ziko katika hatari na bado hazijapata mafunzo haya,” alisema Ummy.

Mikoa sita hatarini

Waziri huyo alitoa tahadhari ya ugonjwa huo kwa wananchi wote, hasa mikoa inayopakana na DRC ambayo ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe.

“Hii haiondoi ukweli kwamba, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA) cha Dar es Salaam; Kilimajaro (Kia) na Songwe cha Mbeya kuwa vipo katika hatari ya kuingiza mgonjwa wakati wowote ule,” alisema.

“Kutokana na hali hii wizara kwa kushirikiana na washirika mbalimbali ikiwamo WHO, wanafanya juhudi ili kuhakikisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaopita katika mipaka yetu yote ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa huu hapa nchini.”

Pia aliwaagiza wakuu wa mikoa yote kuitisha kikao cha afya ya msingi (PHC) kujadili jinsi walivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaingia kwenye maeneo yao.

Mikakati ya kukabiliana na ebola

Waziri Ummy alisema Serikali inafanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa ebola kwenye mikoa minane ya Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya, Kigoma, Kagera, Arusha na Kilimanjaro kwa kuainisha uwezo uliopo pamoja na upungufu unaofanyiwa kazi.

“Wizara imeajiri wataalamu wapya 33 ili kuongeza nguvu katika mipaka yetu na tayari wamesambazwa kwenye vituo vya mipakani.”

Alisema Bohari ya Dawa (MSD), imepokea vifaa vyenye thamani ya Sh5 bilioni kutoka WHO na vimeshapelekwa kwenye maeneo husika ikiwa ni pamoja na vifaa kinga kwa watumishi wa afya kwenye maeneo yote nchini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema wananchi wasihadaiwe kuwa kuna tiba ya ebola kwa kuwa hakuna tiba yoyote iliyopatikana.

“Wananchi wasidanganywe mpaka sasa hakuna dawa na kwa watumishi wa afya hakikisheni mnazifunga vyema sampuli za wagonjwa wanaohisiwa ili kuzuia maambukizi,” alisema Dk Ndugulile.