Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yapunguza upimaji wa mabasi kwenye mizani

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Serikali imepunguza upimaji wa mabasi kwenye vituo vya mizani kufuatia vikao na wadau, hatua inayolenga kupunguza foleni, muda wa safari na matumizi ya mafuta, huku mabasi mengi hayatapimwa kila kituo, jambo linalotarajiwa kupunguza gharama na kuboresha huduma kwa abiria nchini.

Dar es Salaam. Mabadiliko makubwa katika mfumo wa usafiri wa abiria nchini yameanza kuonekana baada ya Serikali kupunguza upimaji wa mabasi katika vituo vya mizani, hatua inayolenga kuondoa changamoto za ucheleweshaji wa safari, kupunguza matumizi ya mafuta na kupunguza gharama za uendeshaji.

Uamuzi huo umefuatia mfululizo wa vikao kati ya Serikali na wadau wa sekta ya usafiri wa abiria, vilivyolenga kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali, hususan ongezeko la gharama za uendeshaji baada ya kupanda kwa bei ya mafuta nchini.

Kikao cha dharura kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kilichofanyika Aprili 12 hadi 13, 2026 jijini Dodoma, kiliwakutanisha watendaji wa Serikali na wamiliki wa mabasi ya abiria, ambapo hoja kubwa ilikuwa ni muda mwingi unaopotea kwenye mizani na athari zake kwa safari za abiria.

Baada ya majadiliano hayo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ilitoa maelekezo mapya kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ambapo Kaimu Katibu Mkuu, Dk Charles Msonde, katika barua ya Aprili 20, 2026, alielekeza utekelezaji wa mfumo mpya kuanzia Aprili 24, 2026.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo, mabasi ya kisasa yenye mpangilio wa ekseli (axle configurations) aina ya SS D6 na SS DC4S2 hayatapimwa tena katika kila kituo cha mizani, bali yatakuwa na utaratibu maalumu wa usafiri.

Kwa mabasi ya mpangilio wa SS S4, yatapimwa katika vituo viwili tu, kituo cha kuanzia safari na kituo cha mwisho, kwa kuzingatia ratiba zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).

Akifafanua uamuzi huo, Dk Msonde alisema lengo ni kupunguza muda wa kusimama mizani, kupunguza matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji bila kuathiri usalama wa barabara.

“Tunataka kuhakikisha usafiri unakuwa wa haraka zaidi, wenye ufanisi, lakini pia bila kuathiri miundombinu ya barabara,” alieleza katika maelekezo hayo.

Wakati Serikali ikitekeleza mabadiliko hayo, wadau wa sekta ya usafiri kupitia Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) wameipokea hatua hiyo kwa mikono miwili, wakisema inaleta nafuu kubwa kwa sekta hiyo na kwa abiria.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumapili, Aprili 26, 2026, Katibu wa Taboa, Priscus John, amesema awali mabasi yalilazimika kusimama mara kwa mara kwenye mizani, jambo lililosababisha foleni kubwa na ucheleweshaji wa safari.

“Kwa sasa mfumo umeboreshwa, mabasi mengi hayatapimwa kila mizani kama zamani. Hii imepunguza muda wa safari na gharama za mafuta,” amesema John.

Amefafanua kuwa mfumo wa zamani ulikuwa na changamoto kubwa kutokana na asili ya abiria kubadilika kila siku, hali iliyofanya upimaji kuwa mgumu na wakati mwingine kuonekana kama kero kwa wasafiri.

“Kwa lori unaweza kupanga mzigo kwa kilo, lakini kwa abiria leo ni wazito, kesho ni wepesi, hivyo upimaji ulikuwa mgumu na mara nyingine uliathiri ufanisi wa safari,” amesema.


Kwa mujibu wa Taboa, mabadiliko hayo yamepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano kwenye mizani, kupunguza gharama za mafuta na kuboresha muda wa safari, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa huduma kwa abiria.

Akilinganisha na nchi jirani, John amesema mfumo kama huo tayari unatumika katika baadhi ya nchi ikiwemo Kenya, ambako mabasi hayapimwi mara kwa mara kama ilivyokuwa Tanzania.

Amesema hatua hiyo ni suluhisho la usawa kati ya maslahi ya watoa huduma na ufanisi wa usafiri wa umma, huku Serikali ikiendelea kusimamia usalama wa barabara.

Kwa upande wa abiria, mabadiliko hayo yamepokelewa kwa furaha. Abiria wa Mwanza, Marygrace Malembela, amesema safari sasa zimekuwa za haraka zaidi na zenye utulivu.

“Sikujua kama kuna utaratibu wa kutokupima katika mizani. Tulikuwa tunaulizana ndani ya gari, maana tuliingia Vigwaza, baada ya hapo sijaona tena mizani, labda nikifika mwisho wa safari,” amesema Marygrace.