Serikali yashtushwa na udumavu wa watoto Iringa

Iringa. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema katika kila watoto 100 wenye umri chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Iringa, 47 wamedumaa kutokana na lishe duni.

Amesema japo mkoa huo una kila aina ya chakula suala la lishe kwa watoto bado ni changamoto.

Akizungumza katika wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye jimbo la Isimani, Ummy amesema kiuhalisia watoto waliodumaa hawawezi kufanya vizuri kwenye masomo hata kama Serikali imewekeza kwenye elimu bila malipo.

“Ndugu zangu wana Iringa tunapovua samaki tusiuze wote, tuwape lishe watoto. Hizi mboga za majani wapatie na watoto wetu, Iringa kuna kila aina ya chakula lakini hali ya lishe ni mbaya,” amesema Ummy.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Salim Asas amewataka wakazi wa Iringa kuacha kuwapatia watoto wao ulanzi na badala yake, wawapatie maziwa na vyakula vingine vyenye lishe.

“Wanyalukolo tuache kuwapa watoto ulanzi, tupulike? Tujitahidi kuwapatia watoto wetu lishe bora. Tuwape watoto maziwa na vyakula vingine, sio ulanzi,” amesema Asas.

Awali, Rais Samia amesema ni ajabu kuona mkoa huo una changamoto ya udumavu wakati kuna vyakula vya kutosha.

Rais Samia alimuagiza watoto wanatakuwa kupata milo mitano kwa siku na sio mitatu kama ambavyo familia nyingi zimekuwa zikifanya.

“Unamuachia mdogo wake mlo kidogo, unaenda shambani huku nyuma wanagawana wote, kwa muda unaorudi anakuwa amekuwa milo mitatu,” amesema Rais Samia.

Amewataka wakazi wa Iringa kuwekeza kwenye lishe ili watoto wapate afya na kuondokana na tatizo la udumavu.