Serikali yatangaza waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Serikali imetangaza uchaguzi kwa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 huku nafasi za bweni zikiangukia zaidi kwa wanafunzi wa Vijijini

Dodoma. Serikali imetangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 huku ikisema imawapa kipaombele wanafunzi wa vijijini shule za kitaifa za bweni.

Akitangaza uchaguzi huo leo Jumatano Novemba 24, 2021, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu amesema nafasi zinazokwenda kwa wanafunzi wa bweni ni za shule za kitaifa.

Katika upangaji wa mwaka huu wanafunzi wote 907,802 waliofaulu mtihani wamepangiwa kuanza masomo Januari 17, 2022 kwa wakati mmoja baada ya maandalizi ya Serikali.

Upangaji huo hautahusisha wanafunzi wenye ufaulu mzuri zaidi ambao wao watapangiwa kulingana na alama zao na kwa mwaka 2022 wanafunzi waliofaulu zaidi na kupangiwa ni wanafunzi 4188.

"Wanafunzi waliopangiwa shule za bweni za Kitaifa ni 1989 na hapa tumechukua zaidi wanafunzi wa vijijini lakini kwenye majiji na halmashauri tumeangalia sana wenye uhitaji tu," amesema Mwalimu.

Waziri ametoa sababu za kupangiwa zaidi kwa wanafunzi wa vijijini katika shule za bweni za Kitaifa kwamba kunatokana na uamuzi wa Serikali wa kujali wanafunzi wote wapate elimu.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, mpango wa kupanga nafasi hizo unakwenda kusaidia wanafunzi ambao huwa kwenye mazingira magumu na vikwazo ili wasome.

Wakati huo Waziri ametoa agizo kwa wakuu wa shule kote nchi kuacha visingizio vya michango au sare kwa wanafunzi wanaoanza bali waachwe waendelee na masomo huku mambo mengine watakamilisha mbeleni.