Serikali yatoa maagizo ununuzi vifaa vya hospitali

Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel

Muktasari:

Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel amewaaagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kutonunua vifaa vya hospitali bila kuwashirikisha wahandisi wa vifaa tiba waliopo kwenye maeneo yao na kuahidi kuwashughulikia.

Dodoma.  Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel amewaaagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kutonunua vifaa vya hospitali bila kuwashirikisha wahandisi wa vifaa tiba waliopo kwenye maeneo yao na kuahidi kuwashughulikia.

Lengo la maagizo hayo ni kuinua sekta ya wahandisi wa vifaa tiba nchini huku Wizara ya Afya ikitajwa kuja na mikakati mbalimbali ili kuokoa fedha zinazotumika kununua vifaa tiba kutoka nje.

Dk Mollel ameyasema hayo leo Septemba 23, 2022 wakati akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa wahandisi wa vifaa tiba nchini uliofanyika jijini hapa.

Dk Mollel amesema ikiwa wahandisi hao wataimarishwa na idara yao kutambulika wataisaidia Serikali kuokoa mabilioni ya fedha kwenye ununuzi, matengenezo ya vifaa hivyo na kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda nje ya nchi kutibiwa.

Amesema Serikali kwa mwaka 2022 pekee imetumia zaidi ya Sh200 bilioni kununua vifaa vya CT scan machines, MRI, Oxygen machine na X-ray machines.

“Wakati mwingine unakuta kifaa kinauzwa Sh78 milioni alafu kinaharibika na kutengenmeza kwake pengine ni kununua kifaa cha milioni moja tu, ila kwakuwa hatuna utaalamu wa kutengeneza basi inatupasa tuagize tena kifaa hicho kwa Sh milioni 78”amesema Dk Mollel.

Kwa upande wake Samwel Hhayuma ambaye ni mtaalamu wa vifaa Tiba amesema bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi hivyo kuendelea na mazungumzo na Idara kuu ya utumishi kupata wataalamu wengine.