Serikali yawekeza Sh27 bilioni miradi ya TAEC
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania. Picha na Happy Lazaro
By Happy Lazaro, Mwananchi
Arusha. Serikali imewekeza zaidi ya Sh27 bilioni kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya miradi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania.
Hayo yalisemwa leo Jumatano Agosti 04, 2021 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati alipotembelea Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo maabara ya kisasa ambayo itahudumia nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Kipanga alisema kuwa, Serikali imewekeza fedha katika tume hiyo kwa lengo la kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuweza kutoa huduma kwa jamii.
"Katika kutembelea miradi mbalimbali nimeweza pia kupita kwenye hilo jengo la maabara ambalo ni kubwa na la kisasa na zaidi ya Sh10.4 bilioni zitatumika hadi kukamilika, ambapo hadi sasa hivi awamu ya kwanza kiasi cha Sh2.38 bilioni kimeshatumika katika ujenzi huo na nimefurahishwa sana na kasi ya ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu."alisema Kipanga.
Alisema kuwa, kila mmoja anaelewa kwenye mahospitali teknolojia inayotumika kutibu baadhi ya magonjwa ni X-ray, hivyo ili kuweza kuratibu namna ya matumizi ya mionzi hiyo ni lazima tuwe na kituo Kama hicho ambacho kitakuwa kinafanya shughuli hizo sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watalaamu mbalimbali.
"Kama Taifa ni lazima tuweke mikakati endelevu na yakini katika kuhakikisha tunatengeneza kituo kitakachotoa elimu kwa watanzania watakaotumika katika maeneo hayo, hivyo nawaombeni muwe na umoja katika kutekeleza miradi hiyo na mshikane na kuwa kitu kimoja ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo yaliyowekwa kwa ustawi wa nchi yetu ."alisema Kipanga.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Atomiki Tanzania, Profesa Lazaro Busagala alisema kuwa kupitia maabara hiyo wanataka kuhakikisha wameimarika zaidi katika suala zima la mionzi ikiwemo kudhibiti matumizi salama ya mionzi kwani ikitumiwa vyema ina faida nyingi hasa kwenye uchunguzi na tiba ya saratani ,hivyo wanahakikisha wamewakinga wananchi ili wasipate madhara yanayosababishwa na mionzi.
Alisema kuwa maabara hiyo kubwa na ya kipekee inategemewa na nchi za Afrika Mashariki na Kati katika kutoa huduma mbalimbali.
Profesa Busagala aliongeza kuwa katika jengo hilo la maabara wataanzisha chuo ambacho kitakuwa kinafundisha watu wafikie hatua ambayo itawasaidia wasiweze kupata madhara ya mionzi ambapo darasa moja litakuwa na uwezo wa kubeba watu mia sita ambao watafundishwa kwa wakati mmoja.
"Kulingana na mkataba chuo kinatarajiwa kuanza rasmi mwakani kwani hadi sasa hivi ujenzi umefikia asilimia 85 hivyo kitaleta manufaa makubwa Sana kwa wataalamu mbalimbali na hata kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ambao watanufaika nacho."alisema.