Sh13.38 bilioni zaboresha Kilometa 1,178 za barabara Shinyanga

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Shinyanga, Mibara Ndirimbi akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Shinyanga imeboresha miundombinu ya barabara zenye kilometa 1,178 zinazoweza kupitika kwa urahisi wakati wote huku kilometa 277 kati ya hizo zikitengenezwa kwa kiwango cha lami katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23.

Shinyanga. Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Shinyanga imeboresha miundombinu ya barabara zenye kilometa 1,178 zinazoweza kupitika kwa urahisi wakati wote huku kilometa 277 kati ya hizo zikitengenezwa kwa kiwango cha lami katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23.

Akizungumza Septemba 4, 2023 mjini Shinyanga katika mkutano na waandishi wa habari, Meneja wa Tanroads mkoani hapa, Mibara Ndirimbi amesema miongoni mwa miundombinu iliyoboresha katika bajeti hiyo ni ujenzi wa barabara mpya ya Ulowa kwenda wilaya ya Kaliua mkoani Tabora yenye urefu wa kilometa 25.

Ndirimbi amesema Mkoa wa Shinyanga una mtandao wa barabara zenye jumla ya kilomita 1,178 zikiwamo 277 za kiwango cha lami na zilizobaki zikiwa kiwango cha changarawe ambapo lengo la utoaji wa fedha hizo ni kufanya maboresho yatakayozifanya zipitike na kutumika wakati wote bila tatizo lolote.

Meneja huyo amesema Sh2.69  bilioni zilitolewa kutoka mfuko wa barabara  (Road Fund)  kwaajili ya miradi ya maendeleo na tayari makaravati mapya yamejengwa kwenye maeneo korofi.

“Kilomita 270 zilikuwa za wakala wa barabara mjini na vijijini (Tarura) zilipendekezwa kupandishwa hadhi  na Serikali na kupewa Tanroads kwaajili ya maboresho ambapo zilikuwa na hali mbaya  ya kutopitika  kipindi cha mvua,”amesema Ndirimbi

Ametoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo ya barabara na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya barabara pamoja na madareva kuacha kubeba mizigo yenye uzito uliopitiliza, kuweka matuta kiholela na kuharibu barabara.

Mkazi wa Ulowa mkoani hapa, Frora Richard ameishukuru Serikali kwa kuboresha barabara hizo kwani italeta nafuu kwa akina mama ambao walikuwa wanapata changamoto kwenda hospitalini wakati wa ujauzito lakini kwa sasa watasafiri bila usumbufu wowote.

Nao baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mwabomba, Ernest Mpema na Manugwa Mihayo   wamesema changamoto waliyokuwa wakiipata kabla ya matengenezo kuwepo walishindwa kusafirisha bidhaa zao na wajawazito kujifungulia njiani kwani barabara ilikuwa ikijaa maji na kutopitika kabisa.

Naye, Abel Paul amesema wamefurahi kuboreshewa barabara kwani  matuta wanayoweka kwenye barabara ni kuzuia ajali  ambapo madereva wa magari na pikipiki wanaendesha kwa mwendo kasi na kutishia usalama wa watembea kwa miguu.