Sheikh Alhad asema bado yupo benchi, Bakwata ikitimiza miaka 55
Muktasari:
- Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeadhimisha miaka 55 tangu kuanzishwa kwake, likijivunia mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kulinda amani na utulivu nchini.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema hivi sasa amekaa benchi kidogo, lakini huenda Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir atamfikiria kwa sababu yeye anacheza namba nyingi.
Sheikh Alhad ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 17, 2023 katika maadhimisho ya miaka 55 ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mfalme Mohamed VI Kinondoni na kuhudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Seleman Jafo.
“Mzee (Mufti Zubeir) anajua ninacheza namba nyingi, lakini pia ana wachezaji wengi. Lakini ukikaa vibaya naweza nikarudi hapo,” amesema Sheikh Alhad na kuibua kicheko miongoni mwa viongozi, wakiwemo masheikh wa mikoa na wakuu wa taasisi mbalimbali za Kiislamu.
Februari 2023, Bakwata kupitia Baraza la Ulamaa lilitengua uteuzi wa Sheikh Alhad ka\ma Sheikh wa Mkoa na kumteua Sheikh Walid Omar kukaimu nafasi hiyo. Katika maadhimisho hayo mshehereshaji wa shughuli alitangaza kuwa hivi sasa Sheikh Walid ni Sheikh kamili wa mkoa wa Dar es Salaam.
Uamuzi wa kutengua uteuzi huo ulikuja ikiwa imepita wiki moja, tangu kiongozi huyo atangaze kuivunja ndoa ya mtalaamu wa tiba mbadala, Juma Mwaka Juma maarufu Dk Mwaka na mkewe Queen Masanja Januari 25, 2023, kufuatia ombi la mwanamke huyo.
Leo Jumapili Desemba 17, 2023 Sheikh Alhad ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, akitoa salaamu fupi za taasisi hiyo amesema ameitumikia Bakwata kwa kiasi chake na ataendelea kuitumikia kwa maelekezo ya Mufti Zubeir.
Sheikh Alhad amewasisitizia Waislamu kuendelea kumuunga mkono Mufti Zubeir na Bakwata kwa ujumla, akisema ndicho chombo pekee cha Waislamu.
“Kwa uongozi uliotuka wa Mufti wa Tanzania (Sheikh Zubeir), kumekuwa na maendeleo makubwa ndani ya Bakwata, awali kuna vitu havikuwepo lakini sasa hivi vipo.
“Hapa tulipo (Ukumbi wa Mfalme Mohamed VI- Kinondoni), kwa wale wanaoijua Bakwata ni maajabu yaliyotokea. Mufti amefanikiwa kuwaleta watu pamoja, watu walikuwa hawapendani wala kutazama lakini Sheikh Zubeir ameendelea kuwa ni baba mwenye huruma kwa watu anaowaongoza, anawasamehe na kuwalea na hatimaye Baraza limekuwa na sura ya namna hii,” amesema.
Katika maadhimisho hayo, alialikwa pia Mchungaji Richard Hananja aliyeipongeza Bakwata kwa kufikisha miaka 55, akisema si jambo dogo licha ya changamoto mbalimbali ilizozipitia, lakini bado baraza hilo lipo imara.
Kama ilivyo kawaida, Mchungaji Hananja hakuacha kuwavunja mbavu wageni waalikwa alipopewa nafasi hiyo:
“Changamoto ndio maisha, hata ukioa mke kama hakeleketi, huyo sio mke kwa sababu mke lazima akelekete na mume anaudhi ndio raha yake, ukiona kimya, (ndoa) imeshakufa, tayari mpo Kinondoni Makaburini.
“Mke asiyenuna, kila wakati anacheka huyo si mke, umeoa jinni, mke anune,” amesema Mchungaji Hananja huku akiwaacha watu wakivunjika mbavu.
Katika salamu zake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amemweleza Dk Jafo kuwa Bakwata ipo imara na ina watu, ndio maana wamesheherekea miaka 55 tangu kuanzishwa kwa baraza hilo mwaka 1968.
“Pamoja na mambo mengine, Bakwata lengo letu pia kuisaidia Serikali katika masuala ya amani na utulivu, nikuhakikishie mgeni rasmi (Dk Jafo), baraza hili lina watu na tunaisaidia Serikali.
“Kuna watu kazi yao ni kuichonganisha Bakwata na Serikali, mara utasikiaa oooh wale hawaendi vizuri au hawana watu, ebu fikiria toka mwaka 1968 hadi leo bado tupo imara, tuna viongozi kila kata, wilaya na mkoa, utasema hatuna watu,” amehoji Sheikh Zubeir.
Sheikh Zubeir alisema Bakwata si chombo au taasisi ya kuandamana bali inafanya shughuli zake kwa taratibu ili kuisaidia Serikali.
“Mheshimiwa mgeni rasmi (Dk Jafo), Bakwata ndio chombo chenu cha kusimamia Uislamu. Kama mtu ana maoni au fikra, basi aje Bakwata si kuzungumzia kando,” amesema.
Awali, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Nuhu Mruma alizungumzia mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa ndani ya miaka 55 hususan katika kipindi cha uongozi wa Mufti Zubeir ulioanza mwaka 2015.
“Tumefanikiwa kuimarisha uhusiano na mataifa mengine ya nchi za nje, hatua iliyoleta tija kubwa hapa nchini, tumeboresha kitengo cha Hijjah na huduma za kijamii,” amesema Sheikh Mruma.