Siku ya mwisho Rais Magufuli kuonekana hadharani

Siku ya mwisho Rais Magufuli kuonekana hadharani

Muktasari:

  • Februari 27 mwaka huu, ilikuwa siku ya mwisho kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli kuonekana hadharani ndivyo unavyoweza kusema.

Dar es Salaam. Februari 27 mwaka huu, ilikuwa siku ya mwisho kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli kuonekana hadharani ndivyo unavyoweza kusema.

Siku hiyo Rais Magufuli alikuwa akimuapisha Dk Bashiru Ally baada ya kumteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi ya Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu hakuzungumza lolote isipokuwa Dk Bashiru ambaye alitoa salama zake baada ya uteuzi huo.

Baada ya hafla hiyo, Rais Magufuli hakuonekana tena, hadi jana, Jumatano Machi 17, umma wa Watanzania ulipotangaziwa kuwa amefariki dunia baada ya kuugua maradhi ya moyo.

Siku ya mwisho Rais Magufuli kuonekana hadharani

Kifo cha Rais Magufuli kilitangazwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kupitia Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), ambapo alieleza kiongozi huyo wa nchi amefariki dunia katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.