Siku ya vijana na kilio cha ajira nchini, suluhisho latajwa
Muktasari:
- Siku ya kimataifa ya vijana huadhimishwa kila mwaka Agosti 12 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu changamoto na fursa zinazowakabili vijana kote ulimwenguni.
Dar es Salaam. Wakati ulimwengu akiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana (IYD), kesho Agosti 12, 2025, wadau mbalimbali wameeleza ukosefu wa ajira na kipato ndiyo changamoto kubwa inayowakabili vijana wa Kitanzania kwa sasa.
Siku ya Kimataifa ya Vijana huadhimishwa kila mwaka Agosti 12 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu changamoto na fursa zinazowakabili vijana kote ulimwenguni. Inatumika kama jukwaa la kukuza ushiriki wa vijana na kusherehekea mchango wao katika jamii, maendeleo na amani.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Vitendo kwa Vijana wa Ndani kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) na Zaidi”, Inaangazia jukumu la kubadilisha jamii walilonalo vijana katika kufikia malengo hayo.
Kaulimbiu hiyo inatambua kuwa vijana si tu wanufaika wa maendeleo, bali ni wahusika wa mabadiliko, ubunifu, na uongozi.
Changamoto ya ajira
Akizungumzia Siku ya Kimataifa ya Vijana, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema ukosefu wa ajira na uwezo wa vijana kujipatia kipato ni changamoto kubwa inayowakabili vijana kwa sababu ya kauli kuwa ‘vijana ni taifa la kesho’, lakini wengi wao hawana uhakika wa kipato chao.
Amesema vijana wengine wamepoteza matumaini ya kesho yao na wanatumia muda mchache kwa uzalishaji, ambapo kati ya saa nane za uzalishaji kwa siku, wengi wanatumia wastani wa saa tatu pekee.
“Maana yake ni kwamba mtu huyo ukimlinganisha na yule anayetumia saa nane kuzalisha, anayetumia saa zaidi ana uwezo mkubwa wa kujikwamua kiuchumi kuliko huyu anayefanya kazi kwa saa chache kwa sababu kipato kinatokana na kiasi cha muda unaofanya kazi,” amesema.
Mkude ameongeza kwamba kama Taifa, Tanzania inapoteza saa nyingi za uzalishaji, jambo ambalo athari zake zinaonekana kwenye Pato la Taifa (GDP) na pato la mtu mmoja mmoja kwani linakuwa chini.
Ili kuondokana na changamoto hiyo, Mkude amesema Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo hazijatumika vizuri, hususan katika sekta ya kilimo kwani kuna ardhi kubwa na vyanzo vya maji vya uhakika, hivyo vijana wanahitaji kusaidiwa mitaji ili waweze kuzalisha.
“Ukiangalia ule ukanda wa Kagera, kuna Mto Kagera na Ziwa Victoria, lakini maji yanayopatikana huko hayajatumika vya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Ni Kagera Sugar pekee ndiyo wanatumia maji hayo kwenye mashamba yao ya miwa.”
“Mtu akihitaji kulima, anahitaji vitu viwili; ardhi yenye rutuba na maji ya uhakika. Siku hizi ardhi yenye rutuba unaipata tu, kuna mbolea nyingi kwa ajili hiyo. Kingine kinachoongezeka hapo ni mkopo, ili kupata mtaji kwa ajili ya kilimo cha kisasa,” amesema.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema changamoto kubwa inayokumba vijana nchini kwa sasa ni suala la ukosefu wa ajira, kwani kwa mujibu wa takwimu za Ripoti ya Nguvu Kazi 2021 na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya 2007 toleo la 2024 inasema kwa mwaka vijana 1,000,000 huingia kwenye soko la ajira.
Hata hivyo, amesema ripoti hiyo inaonyesha kuwa ni vijana 200,000 tu ndio hupata ajira katika sekta rasmi ikiwamo ya umma au binafsi kama vile ualimu, uuguzi, viwandani, kwenye kampuni n.k.
“Vijana takribani 800,000 kwa mwaka wanaachwa nje ya mfumo wa uzalishaji na ajira huku wakiishia kuwa tegemezi na wengine wakiamua kujiajiri na kuingia kwenye sekta isiyo rasmi kama bodaboda, mama lishe, machinga na wengine ambao hawa hawajui hatima yao, hawana uhakika wa kesho yao na hawana sehemu za uhakika kwa shughuli zao,” amesema Nondo.
Ameongeza kuwa vijana wachache walio kwenye sekta rasmi, kazi wanazofanya sio za staha ni hohehahe, wanalipwa mshahara kidogo ambao hauwawezeshi kupiga hatua yoyote zaidi ya kulipa nauli, kodi ya nyumba ya kawaida na kula chakula cha kawaida.
“Wengi kazi zao hazina mikataba, hawana bima ya afya, mishahara yao kuchelewa, hawana mfumo wa akiba kupitia mfuko ya hifadhi ya jamii. Wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi,” amesema.
Nondo amedai hapa nchini kuna jumla ya wahitimu wa fani ya ualimu 146,000 waliopo mtaani bila kazi huku shule zote nchini zikiwa na uhaba wa walimu 279,202. Amesema Serikali ikiajiri wahitimu wote hao 146,000, bado kutakuwa na uhaba wa walimu 133,202.
Kwa upande wake, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Florian Simba amesema tangu amehitimu shahada ya biashara, miaka mitatu iliyopita, hajafanikiwa kupata ajira na siyo yeye pekee, bali na wengine katika darasa lao.
“Kwa sasa nafanya biashara zangu ndogondogo, lakini ukweli sina ajira rasmi, hiyo ndiyo changamoto kubwa. Nina uwezo wa kufanya kazi lakini kazi hakuna, nimefanya usaili mara kadhaa lakini sijafanikiwa,” amesema Simba.
Ameongeza kuwa siku hiyo iwe na ajenda mahususi ya kuwasaidia vijana kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa kuzisukuma serikali za nchi mbalimbali duniani kuweka mazingira wezeshi ya kuwaajiri.
Mikakati ya Serikali
Hata hivyo, katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2025/26, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali imeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzalisha fursa za ajira nchini kupitia uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki, reli ya kisasa, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Vilevile, alisema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kupanua wigo wa uzalishaji wa ajira nchini. Kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Februari, 2025 jumla ya ajira 8,084,204 zimezalishwa katika sekta ya umma na binafsi.
Majaliwa alisema uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji nchini umeongeza usajili wa miradi kwenye sekta binafsi kutoka 416 hadi 615.
“Miradi hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.49 ilizalisha ajira mpya 119,717 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024 ikilinganishwa miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 7.95 iliyozalisha ajira mpya 187,355 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025,” alisema Majaliwa.