Simanzi yatawala maziko ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Rais Samia atuma Salamu

Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe Ester Mahawe ukiwa tiyari kwenye eneo la makaburi kwa ajili ya maziko nyumbani kwake eneo la ngaramtoni ya chini jijini Arusha, picha na Bertha Ismail
Muktasari:
- Ester aliyefariki dunia Januari 14, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyoko mkoani Kilimanjaro, amezikwa leo Januari 20 katika makaburi ya familia yaliyoko nyumbani kwake Ngaramtoni ya chini jijini Arusha.
Arusha. Hali ya majonzi na simanzi imetawala katika mioyo na nyuso za mamia ya waombolezaji katika maziko ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe Ester Mahawe (52).
Ester aliyefariki dunia Januari 14, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyoko mkoani Kilimanjaro, amezikwa leo Januari 20, 2025 katika makaburi ya familia nyumbani kwake eneo la Ngaramtoni ya chini jijini Arusha.

Ester aliyewahi pia kuwa mbunge wa viti maalumu Babati Mjini, kabla ya kuzikwa waombolezaji walipewa nafasi ya kuaga mwili iliyofuatiwa na salamu za rambirambi kutoka kwa makundi mbalimbali, kabla ya Ibada fupi ya kumuombea heri iliyoongozwa na watumishi wa Mungu kutoka Kanisa la Waadventista Wasabato.
Akitoa Salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema marehemu Ester alifanya kazi kwa ufanisi na kuwa mfano bora kwa wenzake waliopewa nafasi ya kumwakilisha Rais katika maeneo yao ya kazi.
"Hivyo kila mmoja ahakikishe anabaki kuwa hadithi iliyo njema kwa wale anaowaongoza kwa kila dhamana mnayopewa na muifanye kazi kwa bidii na maarifa ya hali ya juu, hilo ndilo aliloliacha marehemu" amesema Dugange.
Pia amewataka waombolezaji kuendelea kutetea na kupaza sauti kwa jamii kuheshimu waume zao na kuwatetea kama alivyokuwa anahamasisha marehemu Ester.
"Hata mwanamke ukipata gari ya V8 heshimu mwanaume, kama Ester alivyoacha alama na hadithi iliyo njema ya utetezi wa wanaume" amesema.
Mbali na hilo alitoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kwa msiba huo na kuwataka kuendelea kuyaenzi yote mema aliyoyaacha.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amesema marehemu Ester amefariki na kuacha sifa nyingi kwa watu wote walifanikiwa kukutana naye katika nyanja mbalimbali, ambao wanaweza kumwelezea juu ya ucheshi, upendo na heshima kubwa kwa watu wote bila kujali mkubwa wala mdogo au cheo alichokuwa nacho.
"Mimi ni mzee wa Mkoa wa Manyara, Ester namfahamu vizuri ila sijawahi kumuona akija kusalimia akiwa amekasirika, hata kama ameudhiwa atakusalimia akiwa anafurahi hatakasirika hovyo hovyo," amesema Sumaye na kuongeza.
"Lakini pia alikuwa mtetezi wa wanaume na alikuwa anatutetea akiwasema akina mama wenzake na kusema hawa watu wanaoitwa wanaume ni muhimu sana lazima tukae nao vizuri na lazima tuwatunze hasa nyie wakubwa, mkipewa gari aina ya V8 hamfui nguo zao, mnaanza kuwanyanyasa wanaume, haya ni mambo mazuri na wanawake wenye masikio wayafuate".
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe alikokuwa anafanya kazi marehemu Ester, Daniel Chongolo, ametoa pole kwa wafiwa na kusema marehemu alikuwa mtumishi na rafiki yao waliyofanya naye kazi pamoja na ushirikiano mkubwa.
"Sisi kule Songwe tunafanya kazi kama timu hizi dhamana zinapita, tunapendana, tunashirikiana mengine yote ni ziada mwenyezi Mungu hatupi dhamana iwe fimbo kwa wengine, bali anatupa kama daraja la kuvusha wengine na hili Ester aliliishi kwa matendo," amesema.
Amesema marehemu aliheshimu na kuwa balozi na mtetezi wa kweli wa wanaume, na wengi wameshuhudia hilo waziwazi na ameacha deni kwa wakuu wa wilaya na hasa akina mama.
Aidha amesema sasa hivi kuna janga kubwa la watoto wa kiume ambao tunawasemea vibaya huku malezi na makuzi yao yakiwa hayaendani na yale ya watoto wa kike, hivyo kutaka wazazi kuboresha malezi kwa watoto wao wa kiume Ili yaendane na msingi kwani bila hivyo Taifa litakuja kuwa na janga la kizazi kilichoharibika.
"Tumekua na harakati nyingi za kumpigania mtoto wa kike na kuwasahau watoto wa kiume, jambo ambalo si sawa, turudi sasa nao maana wako kwenye hatari kubwa Ili kufanya kizazi chema baadaye" amesema Chingolo.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais Ofisi ya Rais masuala ya wanawake, Angelah Kairuki amesema Taifa limepata pigo na familia imepata pigo kwa kuondokewa na Ester kutokana na mchango wake mkubwa aliyokuwa nao.
"Mimi binafsi niliongea naye sikukuu za Krismasi mwaka jana akiwa amepanga mengi na alionyesha kupambana lakini ameondoka, tutamkumbuka alifanya mengi sana na ameacha alama yake tuyafuate yale mema," amesema.
Historia fupi ya Ester Mahawe
Akitoa historia fupi ya marehemu, Lulu Mahawe ambaye ni mtoto wa marehemu amesema kuwa mama yake amezaliwa Novemba 5,1973 katika kijiji cha Isale wilayani Mbulu mkoani Manyara.
"Marehemu mama yangu ameacha watoto watatu wa kuwazaa na sita wa kuwalea pamoja na wajukuu tisa" amesema Lulu.
Amesema marehemu alipata changamoto ya maradhi ya saratani Agosti mwaka 2023 ambapo alipata huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali nchini India na Tanzania ikiwemo Ocean Road, Muhimbili, Lugalo zilizopo jijini Dar es salaam na hatimaye KCMC mkoani Kilimanjaro.
Ameeleza mama yake alipata wadhifa wa kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Manyara mwaka 2015 hadi 2020 na pia mwaka huohuo alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya siasa mkoa wa Manyara.
Aidha amesema mwaka 2021 alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa na Juni 2021 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma na mwaka 2023 alihamishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, ambapo aliudumu hadi mauti yalipomfika.
Akitoa neno la Faraja kwenye ibada ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Sakina, Gerald Nyakirere amesema kuwa watabaki kumkumbuka marehemu kwa moyo wake wa kujitolea kumjengea Mungu majengo mbalimbali.