Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi miaka 10 ya mateso aliyopitia Sikujua

Muktasari:

  • Baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka 10 na maumivu makali, hofu na imani za kishirikina kuhusu uvimbe tumboni, madaktari wamefanikisha kutoa uvimbe wenye uzito wa kilo 13 kwenye mfuko wa uzazi.

Mbeya. Mateso, maumivu na hofu vilikuwa sehemu ya maisha ya Sikujua Sanga (40), aliyeishi na uvimbe wenye uzito wa kilo 13 tumboni mwake uliodumu kwa muongo mmoja.

Katika simulizi yake, Sikujua anasema ungemwona akiwa na hali hiyo, ungedhani ni mjamzito aliyebeba zaidi ya pacha wawili. Mbaya zaidi, aliendelea na hali hiyo kwa miaka 10.

Uzito uliotokana na uvimbe huo ni jambo moja, lakini kasi ya mapigo ya moyo na mabadiliko ya mzunguko wa hedhi ni changamoto nyingine zilizoambatana na hali hiyo.

Sikujua, aliyezungumza na Mwananchi kuhusu magumu aliyoyapitia kutokana na hali hiyo, anasema ilianza rasmi mwaka 2014 kwa kushuhudia mabadiliko kadhaa mwilini.

Mabadiliko hayo, anasema, yalianza kwa tumbo kuongezeka taratibu, huku kasi ya mapigo ya moyo ikiongezeka mara kwa mara.

Kwa hali iliyomkabili, Sikujua anasema kwenda kwa mganga wa kienyeji ndilo lilikuwa chaguo lake la kwanza, baada ya kushauriwa na ndugu, jamaa na marafiki.

“Nilikuwa napata maumivu makali na wakati mwingine mapigo ya moyo yalikuwa yanaenda kasi sana, lakini sikujua chanzo chake, nikaenda kwa mganga wa jadi kupata suluhisho,” anasema.

Anasema hali ilikuwa mbaya zaidi ulipofika mwaka 2015, kwani maumivu yaliongezeka, tumbo likakua zaidi na kila alipofikia siku zake za hedhi tumbo lilitanuka.

“Ilipofika mwaka 2020, mzunguko wa hedhi ulibadilika. Badala ya siku nne, nilianza kuona damu kwa siku tisa, tena ikiwa nzito na nyeusi sana,” anasema.

Kila mabadiliko aliyoyashuhudia katika mwili wake, Sikujua anasema yalimwongezea hofu ya uhai na wakati wote huo aliamini waganga ndio wangekuwa suluhu ya tatizo hilo.

“Watu wengi walidhani nina ujauzito kutokana na ukubwa wa tumbo. Kwa kuwa nilikuwa nimeathiriwa na imani za kishirikina, nilitumia dawa mbalimbali za mitishamba nikiamini ningepona,” anasema.


Ushauri wa mganga

Anasimulia alivyoenda kwa mmoja wa waganga kutafuta tiba. Tabibu huyo wa jadi alimuuliza iwapo amewahi kwenda hospitali kwa uchunguzi wa kitaalamu.

“Baada ya kunisikiliza na kuniangalia, mganga aliniuliza kama niliwahi kwenda hospitali kupata vipimo. Aliniambia tatizo langu halionekani kuwa linatokana na imani iliyojengeka kichwani mwangu, akanishauri nikafanyiwe uchunguzi wa kitabibu,” anasema.

Ushauri huo, anasema, ulimfanya aanze kutafakari upya kuhusu hali yake, ingawa bado alikuwa na hofu ya kufika hospitali na kujua visababishi vya tatizo hilo ndani ya tumbo lake.

Kutokana na hali yake, anasema baadhi ya wanafamilia waliendelea kumshawishi kutafuta huduma hospitalini, lakini hakuwazingatia.

“Ndugu zangu walikuwa wakiumia sana kuniona katika hali ile. Waliniita mara kadhaa kuniambia niende hospitali kwa uchunguzi, na kama ningehitaji upasuaji wangegharimia matibabu ili kuokoa maisha yangu,” anasema.


Alifanyaje uamuzi

Sikujua anasema kufanya uamuzi wa kwenda hospitali haikuwa rahisi kutokana na hofu na maswali mengi aliyokuwa nayo kuhusu chanzo cha tatizo lake.

“Hata hivyo, nilijiuliza nitateseka hadi lini. Agosti 8 mwaka jana nilikwenda kwa ndugu zangu, Kata ya Inyala, ambao walisisitiza nifanyiwe uchunguzi kwa gharama zao. Nilipata ujasiri na kukubali,” anasema.

Alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, anasema alifanyiwa vipimo na kubaini kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa kwenye mfuko wa uzazi wenye uzito wa kilo 13.

“Nilipopata majibu nilishtuka sana kiasi cha presha kupanda. Madaktari walinipa muda wa kutulia kabla ya kupanga siku ya upasuaji,” anasema.


Daktari bingwa aeleza

Akizungumza na Mwananchi, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dk Lukumbodzo Lulandala, anasema walimpokea mgonjwa huyo mwaka jana akiwa na uvimbe mkubwa kwenye mfuko wa uzazi.

“Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa awali, tulibaini alikuwa na uvimbe mkubwa kiasi kwamba kwa mtazamo wa kawaida mtu angeweza kudhani ni mjamzito wa mapacha,” anasema.

Dk Lulandala amesema baada ya tathmini ya kina, timu ya madaktari ilifanya maandalizi ya upasuaji kutokana na ukubwa wa uvimbe huo.


Upasuaji wa saa mbili

Kwa mujibu wa Dk Lulandala, upasuaji huo ulidumu kwa takribani saa mbili na kufanikiwa kuondoa uvimbe wenye uzito wa kilo 13.

“Tulimfanyia upasuaji na kuondoa uvimbe huo kwa mafanikio. Tunamshukuru Mungu kwamba mgonjwa aliamka salama na hadi sasa anaendelea vizuri,” anasema.


Visababishi vya uvimbe

Dk Lulandala anasema uvimbe kwenye mfuko wa uzazi ni tatizo linalowakumba wanawake wengi, hasa wanapovuka umri wa ujana.

“Mwanamke anapofikia umri wa miaka 50, takribani asilimia 70 hadi 75 huwa wamepata changamoto ya uvimbe kwenye mfuko wa uzazi,” anasema.

Anasema ugonjwa huo huwa hauna dalili za wazi katika hatua za awali, ingawa asilimia 30 ya wagonjwa hupata dalili mapema.

Anaeleza mafanikio ya upasuaji huo yametokana na maboresho ya sekta ya afya yaliyofanywa na Serikali kupitia ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na kuongezeka kwa madaktari bingwa.

“Kuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa uwekezaji katika sekta ya afya, ambao umeongeza uwezo wa kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi,” anasema.

Aidha, anawataka wanawake kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini changamoto mapema na kupata matibabu stahiki.

Mkazi wa Nsalaga, Uyole, Jiji la Mbeya, Ester Damian, anaomba elimu zaidi iendelee kutolewa kwa wananchi, hususan maeneo ya vijijini, ili watambue kuwepo kwa huduma za kibingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

“Wananchi bado hawana uelewa. Tuombe Serikali kuwezesha kitengo cha mawasiliano katika hospitali hiyo kutoa elimu na matangazo kupitia vyombo vya habari ili jamii, hususan vijijini, ipate uelewa,” anasema.