Siri mwandishi wa kitabu cha ‘Aya za Shetani’ kuchomwa kisu

Siri mwandishi wa kitabu cha ‘Aya za Shetani’ kuchomwa kisu

Muktasari:

  • Ikiwa imetimia miaka 33 tangu kiongozi wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini atoe ‘fatwa’ ya kumuua mwandishi wa kitabu cha ‘Aya za Shetani’ (The Satanic Verses), Salman Rushdie (75) ameshambuliwa kwa kisu jijini New York nchini Marekani.

New York. Ikiwa imetimia miaka 33 tangu kiongozi wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini atoe ‘fatwa’ ya kumuua mwandishi wa kitabu cha ‘Aya za Shetani’ (The Satanic Verses), Salman Rushdie (75) ameshambuliwa kwa kisu jijini New York nchini Marekani.

Mwandishi huyo raia wa Uingereza mwenye asili ya India, alianza kujulikana na riwaya yake ya pili ya ‘Midnight’s Children’ ya mwaka 1981, ambayo ilipata sifa ya kimataifa, ikiwamo tuzo ya Uingereza ya Booker kwa kuigiza kwake India baada ya uhuru.

Hata hivyo, kitabu chake ‘The Satanic Verses’ kilichochapishwa miaka saba baadaye kilisababisha kutolewa amri ya ‘fatwa’ na Ayatollah Khomeini mwaka 1989, akitaka apewe adhabu ya kifo kutokana na riwaya hiyo, iliyoelezwa kuudhalilisha Uislamu na Mtume Muhammad (SAW).

Rushdie alishambuliwa juzi jukwaani kwa kuchomwa kisu na Hadi Matar, kijana mwenye umri wa miaka 24, ambaye wakati ikitolewa ‘fatwa’ mwaka 1989 alikuwa bado hajazaliwa.

Matar, mkazi wa New Jersey nchini Marekani, alimshambulia Rushdie muda mfupi kabla mwandishi huyo kuzungumzia uhuru wa wasanii mbele ya hadhara katika ukumbi wa michezo wa Taasisi ya Chautauqua kulikofanyika tamasha la fasihi la kifahari.


Alivyoshambuliwa

Polisi wa Jimbo la New York, walisema Rushdie alipata jeraha la kisu shingoni baada ya kushambuliwa na Matar, aliyepanda jukwaani kumfuata Rushdie huku akiwa amefunika uso wake kwa barakoa.

Taarifa ya polisi ilisomeka: “Agosti 12, 2022, saa 11 hivi alfajiri, mshukiwa wa kiume alikimbia kwenye jukwaa na kumvamia Rushdie.

“Rushdie alipata jeraha la kisu shingoni na alisafirishwa kwa helikopta hadi hospitali ya eneo hilo ambako amefanyiwa upasuaji, ila hali yake bado haijajulikana.

Msemaji wa polisi, Andrew Wylie kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema Rushdie anapumulia mashine hospitalini na amejeruhiwa vibaya:

“Habari sio nzuri. Rushdie anaaminika kupoteza jicho, mishipa ya fahamu kwenye mkono wake ilikatika na alichomwa kisu kwenye ini, ambalo limeharibika, huku mtuhumiwa akipata jeraha kidogo kichwani.”

Taarifa hiyo ilisema mtuhumiwa ametambuliwa kwa jina la Hadi Matar (24) kutoka Fairview, New Jersey.

“Saa 10.47 asubuhi (saa za New York), Salman Rushdie alikuwa amewasili jukwaani kwa ajili ya mkutano huo wakati mshukiwa alipopanda jukwaani na kumvamia.

“Polisi wa jimbo hilo wanasaidiwa katika uchunguzi huu na ofisi ya Sharif na pia FBI. Katika hatua hii, bado hakujapatikana maelezo juu ya sababu kamili za mshukiwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.


Jaribio la kumuua Rushdie

Tangu kutangazwa kwa ‘fatwa’ Rushdie amekuwa akilindwa na polisi, lakini wale waliohusika na kitabu chake walishambuliwa, akiwamo mfasiri wake wa Kijapani, Hitoshi Igarashi, aliyechomwa na kitu cha ncha kali na kufa Julai 11, 1991.

Ettore Capriolo, mfasiri wa Kiitaliano, alijeruhuwa vibaya kwa silaha ya ncha kali, jijini Milan mnamo Julai 3, 1991. William Nygaard, mchapishaji wa Norway, alipigwa risasi mara tatu katika jaribio la kumuua mjini Oslow mnamo Oktoba 1993.

Wengine ni Aziz Nesin, mfasiri wa Kituruki, aliyekuwa mlengwa mkuu katika matukio yaliyosababisha mauaji ya Julai 2, 1993 mjini Sivas, Uturuki ambapo watu 37 waliuawa.


Ofa ya fedha

Ayatullah Khomeini wakati akitangaza ‘fatwa’ Februari 14, 1989, pia alitangaza zawadi ya Dola za Marekani milioni 2.8 kwa atakayemuua Rushdie.

Hata hivyo, Machi 2016, Shirika la Habari la PEN America liliripoti kuwa donge nono kwa atakayetekeleza fatwa dhidi ya Rushdie liliongezwa hadi kufikia Dola laki sita za Marekani, sawa na euro 430, 000.

Serikali ya Iran kwa muda mrefu imejitenga na amri ya Khomeini, lakini hisia za kumpinga Rushdie zilibaki.

Mwaka 2012, taasisi ya kidini ya Irani iliyoteuliwa ilitangaza kuongeza zawadi kwa atakayemuua Rushdie hadi kufikia Dola za Marekani 3.3 milioni kutoka zilizoahidiwa awali Dola 2.8 milioni.

Ulinzi Uingereza

Ingawaje Serikali ya Uingereza chini ya Margaret Thatcher ilimpa Rushdie ulinzi, wanasiasa wengi wa vyama vyote viwili walimchukia mwandishi huyo.

Mbunge wa chama cha Labour, Keith Vaz aliongoza maandamano kupitia Leicester muda mfupi baada ya kuchaguliwa mwaka 1989 akitaka kitabu hicho kipigwe marufuku.

Hata mbunge wa chama cha Conservative, Norman Tebbit, alimwita Rushdie “fedhuli mkubwa” ambaye maisha yake ya kijamii yamekuwa na rekodi ya mambo ya kipuuzi-puuzi yanayosaliti malezi yake, dini yake, nchi yake ya kuhamia na utaifa wake wa kuomba.

Mwandishi wa habari Christopher Hitchens alimtetea Rushdie na kuwataka wakosoaji kulaani kitendo cha kutoa ‘fatwa’ badala ya kuilaani riwaya na kumlaani mtunzi wake.

Hitchens aliandika kuwa fatwa hiyo ni ufyatuaji wa wazi wa risasi katika vita vya kiutamaduni dhidi ya uhuru.

Licha ya tamko la suluhu lililotolewa na Iran mwaka 1998, na licha ya tamko la Rushdie kuwa angeacha kuishi kwa kujificha, Shirika la habari la Iran lilitangaza mwaka 2006 kuwa ‘fatwa’ iko palepale, kwani wa kuiondoa ni yuleyule aliyeitoa mwanzo, Khomeini ambaye amekwisha fariki dunia.

Rushdie naye baada ya kutolewa ‘fatwa’ alichapisha taarifa kujibu ‘fatwa’ kwamba: “Kitabu hicho kimsingi hakihusu Uislamu, bali kinahusu uhamiaji, mabadiliko, migawanyiko, upendo, kifo, London na Bombay.”


Familia yake

Rushdie ameoa mara nne, mke wa kwanza ni Clarissa Luard aliyepata naye mtoto mmoja Zafar Rushdie, kabla ya kufariki dunia Novemba 4, 1999, mwingine ni Elizabeth West waliyeishi kuanzia mwaka 1997 hadi 2004 na walipata mtoto mmoja, Milan Rushdie. Pia, alimuoa Marianne Wiggins waliyeishi kuanzia mwaka 1988–1993 na walipata mtoto mmoja aitwaye Lara Wiggins na mkewe mwingine ni Padma Lakshmi aliyeishi naye kuanzia mwaka 2004–2007.