Soko la kidigitali latoa mbinu mpya kwa wakulima

Muktasari:

  • Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), linalosimamia mnada wa kijiditali, limeshauri wakulima nchini kutumia vikundi mbalimbali ili kuwezesha kuingia katika mnada huo na hivyo kuwaongezea uhakika wa masoko, uhuru wa kuamua bei, uhakika wa malipo yao pamoja na kuchochea ushindani.

Dar es Salaam. Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) linalosimamia mnada wa kijiditali limeshauri wakulima nchini kutumia vikundi mbalimbali ili kuwezesha kuingia katika mnada huo ili kuwaongezea uhakika wa masoko, uhuru wa kuamua bei, uhakika wa malipo yao pamoja na kuchochea ushindani. 

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 7, mwaka 2023 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa soko hilo, Godfrey Malekano wakati wa Semina na wahariri wa vyombo vya habari nchini. 

Malekano amesema juhudi zilizofanyika hadi sasa ni pamoja na kufanya tathmini ya mnyororo wa thamani wa biashara ambayo ni ufuta, choroko, kakao, dengu, korosho, Pamba, mifugo, chai na kahawa.

“Juhudi zinaendelea katika mazao ya iliki, mbaazi, mkonge, mifugo hai, nyama, ngozi, nyanya, vitunguu na ndizi, tukiongeza thamani itasaidia sana kukuza soko na manufaa kwa Taifa,” amesema Malekano.

TMX iliyoanzishwa mwaka 2015 chini ya Msajili wa Hazina, ilianza kuunganisha wanunuzi na wauzaji, kufanya biashara ya mikataba ya bidhaa papo kwa papo kidigitali mwaka 2019 kwa bidhaa za madini, mazao, mifugo na nishati ndani na nje ya nchi.

Kati ya mwaka 2019 hadi Agosti mwaka huu, tayari soko hilo limewezesha mauzo ya tani 135,103 zenye thamani ya Sh288 bilioni. Mazao ya kahawa ndio yameendelea kufanya vizuri katika soko hilo kwa miaka miwili mfululizo baada ya kuuza Sh110 bilioni mwaka jana na Sh77.5 bilioni hadi Agosti mwaka huu. 

Akijibu swali kuhusu mpango wa kuingia kwenye ukanda wa soko la Afrika, Malekano amesema mipango ni mingi lakini ukanda huo unakabiliwa na changamoto za miundombinu, vikwazo vya ushuru wa forodha (NTBS), uuzaji wa bidhaa zinazofanana na kukosekana kwa viwango vinavyofanana.

Akijibu swali la mwandishi wa kujitegemea, Peter Nyanje aliyeuliza kuhusu ukuzaji wa masoko ya madini kupitia soko hilo Malekano amesema tayari wameshaanza majadiliano na mamlaka mbalimbali sekta ya madini kwa ajili ya kuingiza masoko hayo kwenye mfumo.

Kwa mujibu wa TMX, soko hilo lilianzishwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya KIkwete kutokana na msukumo wa changamoto za bei za bidhaa kutoakisi bei ya soko, bidhaa hafifu,  vipimo visivyo sahihi, kukosekana uhakika wa malipo, gharama kubwa za miamala na upatikanaji wa taarifa sahihi.

Kwa miaka minne sasa limekuwa na manufaa kwa wakulima na wafanyabiashara kuepuka utapeli, kuepuka gharama za usafirishaji, uhakika wa malipo kwa wakulima na mapato kwa Serikali na halmashauri huku likichechemua uchumi wa viwanda na fedha za kigeni.

Soko hili huleta wanunuzi wengi wa ndani na nje ya nchi ambao sio lazima wafike kwenye soko la bidhaa au nchini kwa kuwa mfumo huo huwawezesha manunuzi popote walipo ndani na nje ya nchi.