Somo la Kiingereza mfupa mgumu la saba

Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani (NECTA), Athumani Amasi akitangaza matokeo ya mtihani wa elimu ya shule za msingi kwa mwaka 2022, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Somo la Kiingereza limeonekana kuwa gumu kwa wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka huu, baada ya asilimia 67 ya watahiniwa kupata daraja D.

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mitihani la taifa (Necta) likitangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022 leo, Kiingereza ndiyo somo lililoonekana kuwa somo gumu kwa wanafunzi wengi.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa leo Desemba Mosi na Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Almasi yanaonyesha kuwa asilimia 67.71 ya watahiniwa wote katika mtihani huo walipata daraja D katika somo la kiingereza.



Matokeo hayo ya kumaliza elimu ya msingi yametangwa leo jijini hapa ikiwa ni baada ya watahiniwa 1,384,186 kukaa katika chumba cha mtihani Oktoba 5 na 6 mwaka huu.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa 912,708 walipata ufaulu wa daraja hilo huku wengine 39,086 wakipata daraja E (Utepe mwekundu wa daraja la I) ambao ni sawa na asilimia 2.90.

“Katika somo la English language jumla ya watahiniwa 59,990 wamepata daraja A (utepe wa kijani daraja la kwanza), watahiniwa 56,569 wamepata daraja B (utepe wa kijai daraja la II) na watahiniwa 279,580 wamepata daraja C.

Hiyo ni tofauti na somo la Kiswahili ambapo ni asilimia 7.74 pekee ya watahiniwa ndiyo waliopata daraja D na asilimia 2.76 wakipata daraja E katika somo hilo.

Watahiniwa wengi katika somo hili walikuwapo katika daraja B, ambapo 552,404 walikuwa katika kiwango hicho cha ufaulu ikiwa ni sawa na asilimia 40.92, watahiniwa 403,825 sawa na asilimia 29.96 walipata daraja A katika somo hilo.

“Katika Kiswahili watahiniwa 250,194 sawa na asilimia 18.56 wakipata daraja C.”