Spika akerwa wabunge kupokea simu bungeni
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiwaonya wabunge kusikiliza simu ndani ya Bunge leo Jumatatu Mei 15, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Usikilizaji wa simu ndani ya ukumbi wa Bunge umemkera Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson na kuwataka wabunge kuacha kitendo hicho kwasababu hakipendezi.
Dar es Salaam. Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amewaonya wabunge kuacha kusikiliza simu ndani ya Bunge na badala yake wakiwa na simu za dharura watoke nje ya ukumbi.
Dk Tulia ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 15, 2023 wakati wabunge wakichangia mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/24.
“Sio heshima kwa Bunge na wanaokuja kujifunza hapa, haipendezi, ukiwa na dharura toka nje milango iko mingi, kazungumze na simu. Rejea kama unasimu ndefu nenda mbali zaidi kazungumze na wapiga kura ukimaliza urejee,” amesema.
Amesema haipendezi kuzungumza na simu bungeni na wengine wamekuwa wanaweka vidude masikioni.
“Sijui hamtaki kumsikia anayezungumza, anayechangia unasikiliza muziki ama mpiga kura, sijui unamsikiliza nani na hili liko kwa wabunge, mawaziri kila mmoja,” amesema.
Amesema watu wanaweka vidude masikioni na kuwataka waende nje ya ukumbi wakapokee simu na wakimaliza warejee bungeni.
“Haipendezi kuzungumza na simu kwenye kikao kama hiki. Niwaombe sana tujizuie kuzungumza na simu bungeni,” amesema.