Spika Tulia aomba jimbo lake ligawanywe

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiagiza Serikali kufanyika tathimini ya kina ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wakati wa kipindi cha maswali na majibu Alhamis Aprili 20,2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Spika wa bunge Dk Tulia Ackson ni miongoni wa wabunge waliowasilisha maombi ya kugawa majimbo yao ili kuwa mawili kutokana na ukubwa na wingi wa watu.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ni miongoni wa wabunge waliowasilisha maombi ya kugawa majimbo yao ili kuwa mawili kutokana na ukubwa na wingi wa watu.

Taarifa hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Hamisi Nderiananga wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.

Katika swali lake Mwakagenda ameuliza ni lini serikali italigawa jimbo la Mbeya mjini ambalo linaongozwa na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kutokana na ukubwa wake.

"Kama Serikali tunatambua lakini nikuhakikishie, Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye ni Spika wetu Tulia ameshawasilisha suala hili na lipo mezani kwahiyo muda utakapofika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatizama pia Jimbo la Mbeya Mjini." Amesema Naibu Waziri Ummy akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Sophia Mwakagenda.

Katika swali la msingi mbunge wa Kilindi Omari Kigua ameuliza ni lini Serikali italigawa Jimbo la Kilindi kutokana na jiografia yake.

Naibu Waziri amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo katika maandalizi mbalimbali  ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

“Hivyo kwa kuzingatia taratibu na vigezo, muda wa kugawa majimbo utakapofika Tume itatoa tangazo rasmi kwa wadau wote wa uchaguzi juu ya kuanza kwa machakato wa ugawaji wa majimbo ili wadau wawasilishe maoni na maombi yao na hivyo kushughulikiwa kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa kikatiba,”amesema Ummy.

Ummya amesema majimbo mengi yameomba kugawanywa lakini mambo yanayotazamwa ni pamoja na ukubwa wa ukumbi wa bunge, idadi ya wabunge wa viti maalumu na jiongrafia za maeneo yaliyoomba kugawanywa.