SUA waja na panya wa kupima corona

SUA waja na panya wa kupima corona

Muktasari:

  • Baada ya mafanikio ya utafiti wa kuwatumia panya kutambua mabomu yaliyofukiwa ardhini na vimelea vya kifua kikuu (TB), watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanasema kuna uwezekano mkubwa wa kuwatumia kutambua maambukizo ya virusi vya corona.

Morogoro. Baada ya mafanikio ya utafiti wa kuwatumia panya kutambua mabomu yaliyofukiwa ardhini na vimelea vya kifua kikuu (TB), watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanasema kuna uwezekano mkubwa wa kuwatumia kutambua maambukizo ya virusi vya corona.

Hayo yamebainishwa na mtafiti mwandamizi na meneja wa Mradi wa Utafiti wa Panya (SUA-Apopo) Dk Georgies Mgode baada ya kutoka kwenye Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu 2021) yaliyohitimishwa juzi jijini Dodoma.

 “Tunaamini panya wanaweza kutambua maambukizo ya virusi vya corona kwa ufanisi mkubwa, maana tumeshaona mafanikio kwenye utambuzi wa ugonjwa wa kifua kikuu.

Kwa vile kila kimelea kina harufu yake na kila ugonjwa unaosababishwa na vimelea una harufu yake, tunaamini panya wanaweza kufanya kazihiyo kwa ufanisi mkubwa,” alisema.

Mtafiti huyo alisema wanatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kuwafundisha panya kusaidia kutambua watu wenye maambukizo.

“Hii itakuwa na manufaa makubwa maana vipimo vya corona kwa sasa ni ghali na vinatoka nje ya nchi, lakini kwa kutumia panya itakuwa rahisi na itapunguza maumivu kwa watu wanaopimwa wakati wa kuchukua sampuli ukilinganisha na vifaa vinavyotumiwa sasa kuwapima wahisiwa wa corona,” alisisitiza.

Aidha, Dk Mgode alisema kutambua maambukizo ya awali ni jambo muhimu, kwani litasaidia watu kujilinda na watakaokutwa na vimelea watahudumiwa mapema, hivyo kupunguza vifo na kusambaa kwa maradhi hayo.

 Alisema kuna wanasayansi wengi ambao baada ya kuona mafanikio ya panya walionao walifanya majaribio ya kutumia pua bandia (electronic nose) kunusa vimelea, lakini hawajafanikiwa.

Dk Mgode aliishukuru Serikali kwa kupitisha matumizi ya panya kwenye hospitali zake kwa makubaliano kuwa majibu yathibitishwe na teknolojia nyingine zinazokubalika kabla majibu hayajatumika hospitalini na imekuwa ikifanyika hivyo kusaidia watu wengi kutibiwa.

Mwaka jana pekee, wagonjwa 2,014 walibainika kuwa na kifua kikuu kwa kuwatumia panyabuku hao.

Imeandikwa na Hamida Sharif