Tabora yatumia Sh321.247 bilioni kujenga barabara
Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Tabora akizungumza na waandishi wa habari juu ya miradi iliyotekelezwa na mkoa huo ambapo miwili kati yake inaunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi.
Muktasari:
- Miradi mitatu ya barabara imetekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Tabora ambapo miwili kati yake inaungabisha mikoa ya Kigoma na Katavi.
Tabora. Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Tabora umetumia Sh321.247 bilioni kutekeleza miradi mitatu ya barabara kiwango cha lami, ambapo miradi miwili kati yake inaunganisha Mikoa ya Kigoma na Katavi.
Pia kati ya miradi hiyo, miwili imekamilika kwa asilimia 100, huku mmoja ukitarajiwa kukabidhiwa Juni 30, mwaka huu ambapo hadi sasa umefikia asilimia 89.62.
Hayo yameelezwa leo Aprili 20 na Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Tabora, Rwegoshora Michael akisema miradi iliyokamilka kwa asilimia 100 ni pamoja na wa Tabora hadi Mpanda (Usesula-Komanga) yenye urefu wa kilometa 117.5.
Pia ujenzi wa barabara ya Nyahua hadi Chaya yenye urefu wa kilometa 85.4 nao umekamilka kwa asilimia 100.
"Kwa upande wa mradi wa Tabora - Mpanda umegharimu Sh165 bilioni, Nyahua hadi Chaya umegharimu Sh117.93 bilioni na yote imeshakamilika kwa mujibu wa mkataba.
Akizungumzia mradi ambao kwa sasa umefikia asilimia 89.62 kati ya Kazilambwa hadi Chagu, amesema hadi Juni 2023 utakuwa tayari na utakwenda kuchochea huduma za usafirishaji bidhaa na abiria.
"Kipande hiki cha barabara ni muhimu kwa sababu kinaunganisha mkoa wa Tabora na Kigoma, katika utekelezaji wa ujenzi wa kilometa 36 hizi, kuna kipande kinahudumia na Tabora na kipande kingine kinahudumiwa na Kigoma," amesema.
Amesema kukamilika kwake kutafanya usafirishaji kuwa rahisi na kuondoa ile adha waliyokuwa wakikutana nayo watu.
Isaya Mosha ambaye ni mhandisi mshauri wa mradi huo amesema kati ya Km36 zinazojengwa, Tabora inahudumia kilometa 26 na kilometa 10 zinahudumiwa na Mkoa wa Kigoma.
"Tunakaribia asilimia 90 katika utekelezaji wa mradi huu tunafurahi kuona kuwa tunafikia mwisho, sisi kama wahandisi washauei tunashirikiana kwa karibu sana na Tanroads ili kuhakikisha tunajiridhisha kuwa kazi hizi zinafanyika kwa kiwango stahiki kwa mujibu wa mkataba," amesema Mosha.
Amesema mradi huo umezalisha zaidi ya ajira 400 kwa Watanzania huku ukienda sambamba na fursa mbalimbali za biashara kama kuuza chakula.
Kwa upande wake Mhandisi Ngoka Mirumbe ambaye ni Kaimu Meneja wakala wa Barabara Kigoma (Tanroads), amesema watahakikisha kipande wanachokisimamia kinakamilika kwa wakati