Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tafiti kufungiwa ‘kabatini’ chanzo kukithiri migogoro ya ardhi-2

Katika toleo la jana, tuliangazia jinsi wananchi zaidi ya 600 katika vijiji vya Marogoro, Yavayava na Mfuru Mwambao, Wilaya ya Mkuranga, Pwani, walivyohangaika kwa miaka sita kupata hati miliki bila mafanikio, licha ya kulipa jumla ya Sh20 milioni, Serikali ikieleza kuwa inajaribu kutatua tatizo hilo kwa kuanza upya mchakato wa upangaji na kutoa elimu.

Leo tunaangazia jinsi kutozingatiwa tafiti kunavyochangia kukithiri kwa migogoro ya ardhi.

Inaelezwa Serikali kutofanyia kazi mapendekezo ya tafiti zinazotolewa na wataalamu wa ardhi juu ya kutatua migogoro ya rasilimali hiyo, ni miongoni mwa chanzo cha tatizo hilo kukithiri nchini.

Hotuba za bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za mwaka 2022/23 na 2024/25 zinaonyesha migogoro ya ardhi iliyopokewa kwa ajili ya utatuzi wa kiutawala imeongezeka mara sita zaidi katika kipindi hicho.

Katika hotuba hizo inaelezwa jumla ya migogoro 1,898 ilipokewa hadi Mei 15, 2022 kwa ajili ya utatuzi wa kiutawala, huku hadi Mei 15, 2024 ikiongezeka na kufikia 11,860.

Licha ya kuwapo mapendekezo ya tafiti nyingi kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi, hazitumiki kutatua changamoto hiyo nchini. Mtafiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HakiArdhi, inayojihusisha na uchechemuzi wa masuala ya ardhi ya Haki Ardhi, Cathbert Tomitho anasema: “Tanzania tuna changamoto ya kuzitumia tafiti, ni kama hatuamini sana katika tafiti. Mamlaka zinahisi labda tafiti hizi ni maoni ya watu binafsi na hawazipi uzito.”

Kauli hiyo inaungwa mkono na mhadhiri katika Idara ya Mipango Miji na Mikoa katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Makarius Mdemu anayesema wasimamizi wengi wa Serikali katika sekta ya ardhi wanaongozwa na maelekezo na kauli za kisiasa na hawazipi kipaumbele tafiti.

“Mara nyingi wahusika wanaosimamia masuala ya ardhi hawatafuti taarifa za kitafiti kuhusu eneo lao, wanaongozwa na maelekezo na kauli za kisiasa,” anasema Dk Mdemu.

Hata hivyo, Serikali inasema inaendelea kufanyia kazi mapendekezo ya tafiti hizo, licha ya wadau kuona kwamba yanachukuliwa kama maoni binafsi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda anasema wanaziheshimu tafiti hizo na wanazitumia, akitaja kliniki ya ardhi inayoendeshwa maeneo mbalimbali nchini kuwa miongoni mwa matunda ya utafiti wa wataalamu wa ndani.

“Tafiti tunaziheshimu sana, tumekuwa na kliniki za ardhi ambazo mwananchi wa chini anapata nafasi ya kuonana na kiongozi wa juu na kumwelezea kero zake kuhusu ardhi, utaratibu huo ni miongoni mwa matunda ya tafiti za wataalamu.

“Tunakaa vikao na Jukwaa la Wataalamu wa Ardhi ambao ni watafiti, wanatushauri mambo mbalimbali kuhusu utawala wa ardhi. Tafiti zao zinatusaidia kujua tunaendaje,” anasema.


Zisemavyo tafiti

Miongoni mwa tafiti zilizowahi kutoa sababu na tiba ya migogoro ni ule uliofanywa mwaka 2018 na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ulioitwa ‘Migogoro ya Ardhi nchini Tanzania: Sababu, Athari na Maazimio.’

Utafiti huo ulibaini takribani nusu ya migogoro ya ardhi husababishwa na mkanganyiko wa mipaka.

Utafiti huo, iliofanywa katika halmashauri nane, ulibaini chanzo kikubwa ni mipaka kati ya watu binafsi au kati ya koo kwa asilimia 41.

Kugombea malisho ya mifugo (asilimia 18), uharibifu wa mali katika ardhi, mfano kuchoma miti, kupitisha mifugo (asilimia 18), mgogoro wa umiliki ardhi unaohusishwa na urithi ndani ya familia au ukoo (asilimia 16) na kukosa hati ya kumiliki ardhi (asilimia saba).

Utafiti huo, uliofanywa katika Halmashauri za Wilaya za Mvomero, Kilombero, Moshi, Njombe, Liwale, Mkuranga, Magu na Kiteto ulihusisha wakazi 1,200.

Mbali ya huo, Chuo cha Mipango kwa kushirikiana na Chuo cha Mtakatifu Francis mwaka 2017 walifanya utafiti wa migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Kongwa, ambao mazingira yake yanalandana na maeneo mengi Tanzania.

Utafiti huo, uliochapishwa katika Jarida la Mipango Miji ulibaini sababu za migogoro ya ardhi wilayani Kongwa ni maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wakulima na wafugaji.

Ilibainika katika utafiti huo kuwa asilimia 23.3 ya migogoro ya ardhi ilitokana na wafugaji kuchunga ng'ombe katika mashamba ya wanavijiji, asilimia 15.3 ilisababishwa na kutokuwa na mipaka sahihi ya ardhi, asilimia 12 ilitokana na ukodishaji wa viwanja mara mbili.

“Asilimia 9.1 imesababishwa na kutokuwa na hati miliki, asilimia 5.8 ilitokana na kunyakua ardhi ya watu wengine, na asilimia 6.2 ilitokana na kuondolewa kwa mipaka,” inaelezwa katika utafiti huo.

Pia ulibaini uwapo wa rushwa miongoni mwa viongozi wa Serikali za vijiji unachochea migogoro ya ardhi, ikiwamo kuuza viwanja bila kufuata utaratibu wa mipango miji.

Naibu Waziri Pinda akizungumzia uwepo wa vitendo vya rushwa, anasema wameanzisha mradi wa kutoa elimu sahihi ili kuzuia tatizo hilo.

“Ni kweli unachokisema ndiyo maana hivi sasa tuna mradi wa kutambua matumizi bora ya ardhi ambao viongozi wa vijiji na wananchi wanapewa elimu sahihi ya mchakato wa kuuza ardhi, na hii inasaidia kabla ardhi haijauzwa kijijini, kikao cha kijiji kifahamu. Inapunguza mianya ya rushwa,” anasema Pinda.

Mbali na sababu zilizotajwa awali, utafiti mwingine uliofanywa na Chuo cha Mipango na Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) mwaka 2022, ulibaini chanzo kingine cha migogoro ya ardhi ni kuongezeka kwa idadi ya watu nchini katika maeneo mbalimbali.

“Sababu ni kutokana na kuongezeka kwa mahitaji au shinikizo la idadi ya watu kwenye ardhi kumesababisha kupungua kwa ukubwa wa ardhi na kuongezeka kwa ushindani wa ardhi, hivyo kusababisha migogoro mbalimbali ya ardhi,” unaeleza utafiti huo.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, utafiti mwingine ulifanywa mwaka 2020 na Manja Andreason, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Copenhagen nchini Denmark, kwa kushirikiana na wenzake ambao ni Watanzania, ulibaini kutokana na changamoto ya ongezeko la idadi ya watu, Tanzania ilianzisha Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995.

Katika kukabiliana na athari za ongezeko la watu katika ardhi, Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 inapendekeza matumizi ya teknolojia bora katika shughuli za kiuchumi, ikiwemo kilimo.

“Kwa kuzingatia ongezeko la watu, kuwe na matumizi bora na yenye tija ya ardhi. Hii ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora katika kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi, ili kuongeza uzalishaji na kuepuka matumizi mabaya ya ardhi,” inasema sera hiyo.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina watu milioni 61.7, ambayo imeongezeka kwa asilimia 37.4 kutoka watu milioni 44.9 mwaka 2012, huku ardhi ikibakia ileile yenye ukubwa wa kilomita za mraba 945,087 kulingana na takwimu katika tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Tanzania ina jumla ya eneo la kilomita za mraba 945,087 kati ya hizo, 61,000 ni maji. Pia kati ya hizo, Zanzibar ina ukubwa wa kilomita za mraba 2,654,” inaelezwa katika utambulisho rasmi wa nchi ya Tanzania uliochapishwa katika tovuti hiyo.

Katika hatua za kumaliza migogoro ya ardhi, utafiti wa Chuo cha Mipango na OUT ulipendekeza usajili wa ardhi kufanyika kidijitali.

“Utafiti unapendekeza usajili wa ardhi unapaswa kuwa kwenye mtandao (kidijitali), ili kuhudumia watu wengi kwa wakati na kuweka kumbukumbu sawa kama ilivyofanyika Rwanda na Afrika Kusini,” inapendekezwa katika utafiti huo.

Pia, utafiti ulipendekeza Serikali chini ya Wizara ya Ardhi na wadau wengine kama vile mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) zinapaswa kuangalia hatua muhimu katika kupanga mikakati kwa kuzingatia ukubwa wa eneo la ardhi, ukuaji wa idadi ya watu na uwekezaji wa kifedha na miundombinu ya kifedha.

Itaendelea kesho ambapo tutazungumzia jinsi matobo ya kisheria yanavyochangia kuendelea kuwapo kwa migogoro ya ardhi.