Takukuru yarejesha Sh11.4 milioni zilizolipwa kwa mtumishi hewa
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 20, 2026. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Wakati akilipwa fedha hizo mtumishi huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi, alikuwa akifanya kazi katika chuo cha Uuguzi Machame, kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini badala ya kituo chake cha kazi alichopangiwa na Serikali.
Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imefanikiwa kurejesha serikalini Sh11.4 milioni, baada ya kubaini kuwa mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi alikuwa akilipwa mshahara bila kuwepo katika kituo chake rasmi cha kazi alichopangiwa na Serikali.
Mtumishi huyo alikuwa amepangiwa kufanya kazi katika Hospitali ya Marangu, lakini wakati akiendelea kulipwa mshahara huo kuanzia Agosti 2022 hadi Juni 2023, alikuwa akifanya kazi katika Chuo cha Uuguzi Machame, Wilaya ya Hai kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 20, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2026, Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Musa Chaulo amesema baada ya kubaini mtumishi huyo walimtaka kurejesha kiasi hicho cha fedha ambacho hakustahiki kulipwa.
"Takukuru Wilaya ya Hai, ilifanya uchunguzi wa mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi aliyelipwa Sh11.4 milioni za mshahara wa Agosti 2022 hadi Juni 2023 bila kuwepo kituo chake cha kazi ambacho ni Hospitali ya Marangu,"amesema Kamanda Chaulo
Amesema, "Wakati akilipwa fedha hizo mtumishi huyo alikuwa akifanya kazi katika kituo cha uuguzi Machame. Baada ya kubaini hayo tulimtaka kurejesha fedha hizo ambazo hakustahili kulipwa, Machi 3, mwaka huu mtumishi huyo alirejesha fedha zote Sh11.4 milioni."
Aidha, amesema baada ya kurejesha kiasi hicho cha fedha hatua nyingine za kisheria zinaendelea dhidi ya mtumishi huyo.
Pamoja na mambo mengine, Kamanda Chaulo amesema katika kipindi hicho, wameokoa Sh2.5 milioni za mapato ya Kijiji cha Uparo, kata ya Kirua Vunjo baada ya kubaini kuwa kijiji hicho kiliingia makubaliano yasiyo rasmi na mmoja wa wawekezaji kijijini hapo.
Amesema, "Makubaliano waliyoingia na mwekezaji huyo yalikuwa ya ulipaji ushuru wa madini ya ujenzi kwa kiwango cha Sh2 milioni kwa 'trip' 300 badala ya Sh15,000 kwa kila 'trip' sawa na Sh4.5 milioni kwa 'trip' 300."