Takukuru yatwishwa ‘mzigo’ kusaka dawa migogoro ya ardhi nchini

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya uchunguzi mwaka 2024 leo Juni 10, 2024 katika shule ya Polisi Tanzania, iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema maeneo ya kutolea huduma nchini bado ni tatizo na sekta ambayo imeiumuza nchi na kuleta migogoro mikubwa kwa familia na jamii ni sekta ya ardhi na kuitaka Takukuru kuitupia jicho kwa karibu ili kuja na suluhisho.
Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetakiwa kuitupia jicho sekta ya ardhi inayoonekana kushamiri migogoro ya ardhi inayotishia ustawi wa wananchi na jamii kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu, Juni 10, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi mwaka 2024, kwa maofisa wa Takukuru katika shule ya Polisi Tanzania, iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Simbachawene amesema maeneo ya kutolea huduma nchini bado ni tatizo na sekta ambayo imeiumuza nchi na kuleta migogoro mikubwa kwa familia na jamii ni sekta ya ardhi, hivyo kuitaka taasisi hiyo kuitupia jicho kwa karibu na kuja na suluhisho.
Amesema kuna haja ya Takukuru kufanya utafiti katika sekta ya ardhi, kubaini chanzo cha migogoro hiyo na kuja na mapendekezo ambayo yataisaidia Serikali kukabiliana na migogoro hiyo.
"Msisitizo wangu, Mkurugenzi wa Takukuru tujikite zaidi maeneo ya kutolea huduma, kwani kuna tatizo kubwa… wapo wenzetu wengine kwa kweli wanageuza sehemu za kutoa huduma kama ndiyo sehemu yao ya kupata kiinua mgongo na utajiri. Na Sekta ambayo imeiumiza nchi hii sana na imeleta migogoro mikubwa sana, kusumbua familia na jamii ni sekta ya ardhi.
"Kila mkoa, kila mahala kuna mgogoro wa ardhi, inadumaza maendeleo na inaharibu malengo ya baadhi ya watu. Unampa kiwanja huyu, halafu unashangaa mtu mwingine amepewa, unakuta hati zinagongana mbili.
“Hivi tunashindwaje kuwatafuta hao wote waliohusika popote walipo waje wajibu?” amehoji Simbachawene na kuongeza;
"Takukuru tusaidieni kwenye hili, kwa sababu migogoro ya ardhi inatengenezwa,halafu watu wanalakamika na viongozi wakipita wanaanza kusuluhisha migogoro na ni kwa sababu ya watu ambao tulikuwa tunawachekeachekea."

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya uchunguzi mwaka 2024 leo Juni 10, 2024 katika shule ya Polisi Tanzania, iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Pia ameitaka Takukuru kushirikiana na vyombo vingine, ikiwemo polisi na Tume ya Maadili kushughulika na wale wanaoghushi nyaraka za ardhi na kujipatia hati miliki kinyume cha sheria.
"Sasa hivi katika maeneo mengi watu wanalalamika, Waziri wa Ardhi anahangaika huko na huku, watu wamegushi nyaraka. Kugushi ni jinai, Takukuru shirikianeni na vyombo, ikiwemo Jeshi la Polisi na Tume ya Maadili, muweke mkakati wa pamoja wa kushughulika na hii sekta ya ardhi," amesema.
Pamoja na hayo, amewataka maofisa wa Takukuru kuongeza kiherehere katika kuzuia vitendo vya rushwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kufuatilia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Simbachawene pia ametumia nafasi hiyo kuwataka wakufunzi wa mafunzo hayo ya awali ya uchunguzi kuweka mkazo kwenye sayansi na mbinu za kuzuia rushwa.
Maofisa wanaopatiwa mafunzo
Awali, akitoa taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni amesema maofisa uchunguzi wanaopatiwa mafunzo ya awali ya uchunguzi ni 310, wachunguzi wasaidizi 110 na watumushi 16 wanabadilisha kada.
Amesema washiriki hao waliwasili shuleni hapo Mei 31, 2024 tayari kwa mafunzo ya awali ya uchunguzi ambayo yatafanyika kwa miezi mitano na kwamba ni ya muhimu na lazima kwa maofisa uchunguzi wote wa Takukuru.
"Kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022, Serikali imeipatia Takukuru vibali vya kuajiri watumishi 1,190, ambapo mwaka 2021/2022 tulipata kibali cha kuajiri watumishi 450 ambapo waajiriwa wapya ni 380 na ajira mbadala 70.
"Mwaka 2022/2023 tulipata kibali cha kuajiri watumishi 320, waajiriwa wapya 250 na ajira mbadala 70 na mwaka 2023/2024 tumepata kibali cha kuajiri watumishi 420 ambapo waajiriwa wapya ni 350 na ajira mbadala ni 70," amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania, Moshi, Ramadhan Mungi, amesema wakufunzi wa shule hiyo kwa kushirikiana na wale wa Takukuru wataandaa maofisa bora wa uchunguzi watakaozuia na kupambana na rushwa kwa maslahi ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka waajiriwa wapya wa Takukuru wanaopatiwa mafunzo kutumia muda waliopewa kujifunza kutimiza kusudi lililokusudiwa na kuisaidia Serikali kupambana na vitendo vya rushwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amewataka Takukuru kutimiza wajibu wao wa kuzuia na kupambana na rushwa, ikiwemo rushwa ya matumizi mabaya ya muda na kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.