Tanesco: Mvua zikichelewa kutakuwa na mgawo wa umeme

Muktasari:

  • Kutokana na upungufu wa maji katika mabwawa wa umeme nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Maharage Chande amesema ikiwa mvua zitachelewa kutakuwa na uhaba wa umeme.

Iringa. Wakati uharibifu wa mazingira ukiongezeka katika maeneo mbalimbali hasa ya vyanzo vya maji, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande amesema ikiwa mvua za vuli zitachelewa kutakuwa na uhaba wa umeme kutokana na kupungua kwa maji.

Hata hivyo amesema kukua kwa teknolojia na ongezeko la viwanda kumeongeza matumizi ya umeme kwa kiasi kikubwa.

Katika Bwawa la Mtera, Kihansi na Kidatu kupungua kwa kina cha maji ni kati ya changamoto zilizojitokeza.

Akizungumza katika ziara ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Chande amesema licha ya matumizi ya umeme kuwa makubwa na maji kupungua siku hadi siku Uzalishaji wa umeme bado upo vizuri.

"Vituo vyetu vinafanya kazi ila tusipopata mvua kutakuwa na upungufu wa umeme na kwa sasa tunaomba mvua zinazotegemewa zinyeshe haraka kwa sababu kama hazitanyesha vituo vyetu vinaendelea kudhusha uzalishaji na tutapata upungufu," amesema nakuongeza;

"Kunapokuwa na upungufu wa umeme unatokea mgao, hali hiyo inapotokea huwa tunawaambia wateja wetu kuwa upungu na ndio maana tunasema mvua zisipokuja mapema kutakuwa na upungufu wa umeme," amesema.

Amesema kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita kumekuwa na kasi ya matumizi ya umeme kwa sababu ya ongezeko la uwekezaji kwenye viwanda.

"Tunaongeza juhudi katika kuhakikisha bwawa letu la Umeme la Mwalimu Nyerere linakamilika kwa wakati na tunaongeza juhudi katika kuzalisha umeme. Bwawa la Mwalimu Nyerere limefikia asilimia 91," amesema.

Chande ameongeza kuwa mpaka Juni mwakani umeme wanza utaanza kupatikana katika Bwawa la Mwalimu Nyerere na majaribio yataanza Februari.

Amesema mwaka jana waliongeza umeme megawati 185 kituo cha Kinyerezi 1 lakini kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi tayari zimetumika zote.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali inafanya jitihada zote kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika.

Amesema hali ya uzalishaji umeme imetengemaa na Serikali kupitia Tanesco inafanya jitihada kuhakikisha Watanzania wanapata umeme.

Kuhusu utunzaji wa Mazingira, Kapindi amesema Serikali chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya utunzaji wa Mazingira.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Usi Salum alisema wameridhishwa na utendaji kazi wa Tanesco na kusisitiza suala la mazingira ili kutunza vyanzo vya maji.