Tani 28 za magendo zakamatwa mpaka wa Tarakea, Rombo
Tani 28 za magendo zilizokamatwa mpaka wa Tarakea, Rombo.
Muktasari:
- Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro imekamata tani 28.15 za zao la makadamia yaliyokuwa yakisafirishwa na kuingizwa nchini kinyume cha sheria katika mpaka wa Tarakea, Wilaya ya Rombo, Mkoani hapa.
Rombo. Katika kudhibiti uingizwaji wa magendo nchini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro imekamata tani 28.15 za zao la Makadamia yaliyokuwa yakisafirishwa na kuingizwa nchini kinyume cha sheria katika mpaka wa Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani hapa.
Akizungumzia kukamatwa kwa magendo hayo leo Mei 5, 2026 , Meneja wa TRA, Mkoani hapa, James Jilala amesema shehena hiyo imekamatwa na Maofisa wa TRA wakati wakiwa kwenye doria za kawaida kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama usiku wa Aprili 29, mwaka huu.
"Shehena hii ilikuwa tayari imepakiwa kwenye magari mawili aina ya fuso mpakani Tarakea, zikitokea nchini Kenya kwa kupitia Lower Road. Shehena hii ilikuwa ikihamishwa kutoka kwenye gari ya Kenya aina ya Mercedes Actros," amesema Jilala
Tani 28 za magendo zilizokamatwa mpaka wa Tarakea, Rombo zikiwa ndani ya lori.
Aidha, amesema hatua za uchunguzi kuhusu shehena hiyo bado zinaendelea na magari hayo pamoja na mizigo vyote viko chini ya Idara ya forodha mpaka wa Tarakea huku taratibu za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa tukio hilo.
Jilala amewataka wafanyabiashara Mkoani humo kufuata sheria na taratibu zote za ufanyaji wa biashara kwa kufuata taratibu na sheria za nchi na kuhakikisha wanatumia njia rasmi za kuingiza bidhaa nchini.
"Tunahimiza wananchi na wafanya biashara kwa ujumla hasa kwenye mkoa wetu wa Kilimanjaro, kutekeleza wajibu sahihi kwenye ufanyaji wa biashara kwa kufuata taratibu na sheria za nchi, hasa kutumia njia rasmi za kuingiza na kuondosha bidhaa nchini,"amesema Jilala
Amesema "Kwenye mkoa wetu wa Kilimanjaro tuna vituo vitatu vya forodha ambavyo ni KIA, Holili na Tarakea, hivyo tunahimiza wananchi kutumia malango haya pindi wanavyoingiza bidhaa nchini au wanapouza bidhaa kwenda nje ya nchi."
Akizungumza mmoja wa wananchi wa mkoa huo, Laurence Apolinary amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa sio waaminifu kwa kutaka kupata faida kubwa kwa kukwepa kulipa kodi na hivyo kuikosedha serikali mapato.
"Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na tamaa za kujipatia mali kwa njia ya magendo na hii imekuwa ni changamoto kubwa hasa kwenye maeneo ya mpakani, ukiangalia Wilaya ya Rombo ina vipenyo vingi kwa hiyo watu wanatumia fursa hiyo kupitisha magendo," amesema mwananchi huyo.