Tanroads kuboresha hadhi ya Jiji la Dodoma
Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu alizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea miradi inayotekelezwa na ofisi hiyo.
Muktasari:
- Wakati kilometa 45 za lami zikitarajiwa kujengwa katikati ya Jiji la Dodoma na Km50 katika Wilaya ya Mpwawa wananchi wamesema inasaidia kuchochea uchumi binafsi.
Dodoma. Katika kufanya maboresho na kuongezea hadhi ya makao makuu ya nchi kilometa 45 za barabara ya kiwango cha lami zinatarajiwa kujengwa katika barabara zinazopatikana katikati ya jiji la Dodoma.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 18, 2023 na Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu
baada ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya mkoa huo.
Chimangu amesema Tanroads tayari usanifu unaendelea wa barabara na nyingine zinazotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibu.
"Katikati ya Jiji la Dodoma zaidi ya kilometa 45 za barabara kiwango cha lami zinakwenda kujengwa, miradi hii mingine inaanza kutekelezwa kuelekea baadhi ya Wilaya za Mpwapwa ambapo tutajenga kilometa 50 za lami.”
Mbali na hilo pia barabara inayoelekea katika Hospitali ya Mvumi imeanza kujengwa ili kurahisisha ufikiahi wa huduma kwa watu.
Wakizungumzia miradi inayotekelezwa, baadhi ya wananchi wamesema mbali na kuchochea uchumi wa mkoa pia unarahisisha ufikiaji wa huduma mbalimbali.
"Kidogo tutakuwa katika hadhi ya Jiji, maana ilikuwa haipendezi baadhi ya barabara kuwa mjini lakini hali yake hairidhishi hasa kipindi cha mvua inakuwa shida," Mabena Magawa mkazi wa Nanenane aliiambia Mwananchi digital.
Rahel Nchagwa amesema uboreshaji huo wa miundombinu unawasaidia katika urahisishaji wa shughuli za kiuchumi kwa kurahisisha ufikiaji wa huduma.
"Inakuwa rahisi kufuata bidhaa kwa ajili ya kuuza kwa wateja wetu sisi kama wachuuzi wadogo, badala ya kutumia saa 2 barabarani ikiwa imetengenezwa vizuri nusu saa inatosha na ule muda tuliopoteza awali tunatumia kufanya biashara," amesema Rahel.