Tanzania, DRC kuimarisha usafirishaji mizigo Ziwa Tanganyika
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Eric Hamissi (kushoto) akiwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Taifa ya Meli ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Lignes Maritimes Congolaises – LMC), Frank Banze Nkulu (kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa usafirishwaji Ziwa Tanganyika. Picha na Saada Amir
Muktasari:
- Hati ya makubaliano hayo imeanza kutekelezwa baada ya kusainiwa na itakuwa ya miaka mitatu, huku tathimini ikiendelea kufanyika ili kuimarisha na kupanua maeneo ya ushirikiano.
Mwanza. Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) na Kampuni ya Taifa ya Meli ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Lignes Maritimes Congolaises (LMC) zimesaini makubaliano ya miaka mitatu ya kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara ya kikanda na kuunganisha masoko ya Afrika Mashariki na Kati.
Makubaliano hayo yanahusisha ushirikiano katika kukuza usafiri kwa njia ya maji, kuboresha huduma za usafirishaji wa shehena na abiria pamoja na kubadilishana utaalamu na uzoefu katika sekta ya ubaharia kati ya kampuni hizo mbili.
Akizungumza Juni 15, 2026 wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Tashico, Eric Hamissi amesema makubaliano hayo ni hatua ya kimkakati inayolenga kujenga uwezo wa kitaifa katika usafirishaji wa majini na kuongeza ushiriki wa Tanzania katika biashara ya usafirishaji wa shehena kimataifa.
Amesema kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika kwa kupanua soko la huduma za usafirishaji, huku ikiimarisha nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati hususani DRC.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Eric Hamissi akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa usafirishwaji Ziwa Tanganyika kati ya Tanzania na Congo. Picha na Saada Amir
“Huu ni ushirikiano unaotokana na uhitaji wa pamoja....tunataka kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa majini na kuhakikisha tunatumia kikamilifu fursa zilizopo katika ukanda wa Ziwa Tanganyika,” amesema Hamissi.
Kwa mujibu wa Hamissi, makubaliano hayo pia yatawezesha kubadilishana utaalamu kati ya pande hizo mbili, ambapo LMC ina uzoefu mkubwa wa usafiri wa baharini kupitia Bahari ya Atlantiki, huku Tanzania ikiwa na uzoefu katika usafiri wa maziwa makuu.
Amesema kwa kuanzia, kampuni hizo zinatarajia kuanza na matumizi ya meli za kukodi ili kukidhi mahitaji ya soko, huku mipango ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kujenga na kumiliki meli za pamoja zitakazohudumia biashara katika ukanda huo.
“Tunalenga kufikia hatua ya kuwa na meli zetu zitakazobeba mizigo kutoka masoko ya kimataifa na kuileta moja kwa moja katika nchi zetu,” amesema.
Makubaliano hayo yanakuja wakati ambapo Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuimarisha nafasi yake katika kuhudumia mizigo ya nchi jirani, ikiwemo DRC ambayo ni miongoni mwa wateja wakubwa wa bandari hiyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya mizigo ya DRC hupitia Tanzania, jambo linaloifanya nchi kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa LMC, Frank Banze Nkulu amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na DRC.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Taifa ya Meli ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Lignes Maritimes Congolaises – LMC), Frank Banze Nkulu akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa usafirishwaji Ziwa Tanganyika. Picha na Saada Amir
Amesema ushirikiano huo unalenga kujenga mfumo wa kisasa na wenye ufanisi wa usafirishaji utakaokidhi mahitaji ya wafanyabiashara na jamii zinazozunguka Ziwa Tanganyika.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tashico, Meja Jenerali Mstaafu, John Mbunge amesema makubaliano hayo yataisaidia Congo kupunguza utegemezi wa usafirishaji wa mizigo kupitia Bahari ya Atlantiki na badala yake kuimarisha matumizi ya njia ya Bahari ya Hindi kupitia Tanzania.
Amesema hatua hiyo itaziwezesha kampuni hizo kufikia masoko ya dunia kupitia bandari za Tanzania, huku zikichangia kuongeza ushindani wa huduma za usafirishaji.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Manchali Suguta amesema uwekezaji katika sekta ya usafirishaji ni muhimu katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Naye, Nahodha Adamu Mwisungu amesema ushirikiano huo utasaidia kubadilishana ujuzi kati ya wataalamu wa pande hizo mbili, jambo litakaloboresha huduma za usafiri wa majini.